Thursday, 30 January 2014

Mkuya: Serikali itaendelea kukopa

Pia ameelezea sababu  za kuongezeka kwa deni la taifa kuwa ni mikopo iliyopokewa na serikali na ambayo muda wake wa kulipa haujafika kutoka vyanzo vya masharti nafuu ya kibiashara pamoja na malimbikizo ya riba ya deni la nje.
Waziri Mkuya alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam jana alipozungumza na waandishi wa habari kuelezea utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Fedha.
Alisema hadi kufikia Desemba mwaka jana, deni la taifa lilikuwa limefikia dola bilioni 17.10 sawa na sh trilioni 27.04
Alisema deni hilo linajumuisha deni la nje dola bilioni 12.79 sawa (sh trilioni 20.23) na deni la ndani ni sh trilioni 6.81 ambazo ni sawa na asilimia 25.19 ya deni la taifa.
Kati ya deni la nje la taifa, dola bilioni 10.563 (sh trilioni 16.71) na deni la sekta binafsi ni dola bilioni 2.23 sawa na trilioni  3.52.
Mkuya alisema licha ya deni la taifa kuongezeka kwa kasi nchini lakini mfumuko wa jumla wa bei umeendelea kushuka hadi kufikia asilimia 5.6 Desemba mwaka jana ukilinganisha na asilimia 19.8 zilizofikiwa Desemba mwaka juzi.
“Kupungua kwa mfumuko wa bei kulitokana na sera thabiti za fedha na kibajeti pamoja na kuimarika kwa uzalishaji na usambazaji wa chakula nchini suala hili limekuwa likielezwa kwa kina na Ofisi ya Taifa ya Takwimu  katika taarifa za kila mwezi,” alisema.
Kuhusu matumizi ya mashine za kielektroniki, alisema utaratibu huo utaendelea kutumika kama kawaida na kusimamia vema katika kukusanya kodi ili kuongeza pato la taifa na kupunguza ukwepaji kodi.
“Tulikubaliana na viongozi wa wafanyabiashara  kuwa muda wa kuanza kutumia mashine usogezwe  hadi kufikia tarehe 30, Januari 2014, ili kuwapatia wananchi muda wa kutosha kujiandaa na utekelezaji wa matumizi hayo ya mashine,” alisema Mkuya.

Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment