SAMUEL Eto’o anakumbuka mara ya kwanza alipomwona shujaa wake wa
kwenye soka. Kipindi hicho, Eto’o alikuwa na umri wa miaka minane tu,
akawa anakwenda uwanjani Douala kumshangaa Roger Milla kwenye mazoezi ya
timu ya taifa ya Cameroon.
Hiyo ilikuwa miezi michache tu kabla ya Milla kwenda kwenye fainali za Kombe la Dunia mwaka 1990 zilizofanyika Italia.
Uwanjani hapo kwenye mazoezi, Eto’o alishinda
kutwaa nzima, kuanzia saa 2 asubuhi hadi saa 10 jioni ili tu amwone
Milla. Straika huyo mkongwe, alichokuwa akifanya ni kutabasamu tu kila
alipomtazama Eto’o.
Milla alikuwa akionyesha ujuzi wake ndani ya
uwanja, akawa anapandisha soksi zake kabla ya nyingine kwenda
kuzitundika kwenye uzio karibu na ulipokuwa mkono wa baba yake Eto’o.
Akiwa mtoto, Eto’o alibaki kushangazaa tu, huku Milla alimpungia mkono
kila mara.
“Nilisubiri kwa muda mrefu sana kumtazama na
nilipomwona ilikuwa furaha kubwa sana kwangu. Alikuwa shujaa wangu,”
anasema Eto’o akimzungumzia Roger Milla, mwanasoka mashuhuria Cameroon
na Afrika kwa ujumla.
Wakati Eto’o akikumbuka hilo lililowahi kumtokea
utotoni na jinsi alivyopambana kutimiza ndoto zake kuwa kweli, wiki
iliyopita hadithi ilibadilika na yeye kukawa na mtoto anayemhusudu na
kuwa shujaa wake.
Alipokuwa mazoezini, Eto’o alipata ugeni wakati alipotembelewa na mtoto, Nathan Thomas, ambaye straika Eto’o ndiye shujaa wake.
Mtoto Nathan ana umri wa miaka 10 na anasumbuliwa
na ugonjwa wa ini, lakini mara zote amekuwa akimfuatilia Eto’o kwenye
klabu zote anazocheza tangu akiwa Inter Milan, Anzhi na sasa Chelsea.
Nathan si shabiki wa Chelsea, bali ni shabiki wa
Eto’o na hilo limetokea baada ya kumwona kwenye michezo ya kompyuta
wakati huo alipokuwa akiichezea Barcelona ya Hispania.
Tangu hapo mtoto Nathan akawa anamfuatilia Eto’o
kwa kila hatua akihama kutoka Hispania kwenda Italia, Urusi na sasa yupo
England.
Ndoto kubwa ya Nathan ni kwamba siku moja aonane
na Eto’o ana kwa ana, kitu ambacho wiki iliyopita kilitimia. Nathan
alipata nafasi ya kwenda uwanjani Stamford Bridge Jumapili iliyopita
kutazama mchezo wa Ligi Kuu England kati ya Chelsea na Manchester
United. Kwenye mchezo huo, wenyeji Chelsea waliitandika Manchester
United mabao 3-1.
Kitu cha bahati kwa Nathan ni kwamba shujaa wake, ambaye ni
Eto’o alifunga ‘hat-trick’ kuing’arisha Chelsea uwanjani hapo. Baada ya
kumshuhudia aking’ara uwanjani, siku chache baadaye mtoto Nathan
alitembelea kwenye mazoezi ya Chelsea huko Surrey na akamwona shujaa
wake, ambaye baadaye walifanya mazoezi ya pamoja.
Nathan, alifika kwenye viwanja hivyo vya Chelsea
akiwa amevaa jezi ya Inter Milan iliyokuwa na jina la ‘Eto’o 9’
mgongoni. Akafanya mazoezi na staa huyo wa Cameroon kabla ya kupewa jezi
nyingine ya Eto’o ya Chelsea yenye namba 29 anayovaa kwa sasa.
Mtoto Nathan alifika mazoezini hapo akiwa na wazazi wake, Mel na Debbie na mdogo wake wa miaka saba, Aiden.
Familia hiyo ilitazama mazoezi ya Chelsea kwanza
kabla ya Eto’o kufanya mazoezi ya kivyake na mtoto huyo kwa kipindi cha
dakika 20 katika uwanja wa ndani.
“Sifahamu ni nani aliyefurahi zaidi mimi au
Nathan,” alisema Eto’o, baada ya kusaini mpira, jezi na kisha kumpa
mtoto huyo kama zawadi.
Lakini, Eto’o pia aliipa mwaliko familia hiyo
kwenda Stamford Bridge jana Jumapili kushuhudia mechi ya raundi ya nne
ya Kombe la FA ambapo Chelsea ilitarajia kumenyana na Stoke City.
Baada ya kuifunga mabao matatu Manchester United,
Eto’o alifichua jinsi alivyomshawishi kocha Jose Mourinho na
kumwaanzisha kwenye mchezo huo licha ya kikosi hicho kuwa na mastraika
wengine wakali, Fernando Torres na Demba Ba.
Eto’o na Mourinho walishawahi kufanya kazi pamoja
wakati walipokuwa na kikosi cha Inter Milan ya Italia ambapo waliweza
kunyakua mataji matatu kwa msimu mmoja, Serie A, Kombe la Italia na Ligi
ya Mabingwa Ulaya mwaka 2010.
Kwenye kikosi cha Inter, Eto’o alikuwa
akishirikiana na Diego Milito kwenye safu ya ushambuliaji iliyoifanya
timu hiyo kuwa tishio na kuzitambia timu nyingi ikiwamo Barcelona
iliyokuwa kwenye ubora wake kipindi kile.
No comments:
Post a Comment