Tuesday, 28 January 2014

Mwasikili: Nimewafaidi sana Wazungu

BEKI wa kati na nahodha wa timu ya Taifa ya Wanawake ‘Twiga Stars’, Sophia Mwasikili amemaliza mkataba wake na  Luleburgaz ya Ligi Kuu ya Wanawake ya Uturuki na kurejea nchini.
Mchezaji huyo amezungumza na Mwanaspoti na kufafanua kiundani hali halisi ya maisha yake ya Ulaya na alivyo sasa nchini.“Kwanza sitaki kufanya starehe kwa sasa ingawa kipindi cha nyuma nilizifanya sana, natengeneza maisha labda uzeeni ndiyo nitarudia tena kujirusha, siku hizi baada ya mazoezi huwa napendelea zaidi kulala.
“Niliamua kupunguza marafiki wa aina hiyo baada ya kuona hawana maana kikubwa ilikuwa ni kurudishana nyuma kwani tulikuwa hatufanyi mambo ya muhimu,” anasema Mwasikili na kuonyesha tofauti kubwa ya soka la Uturuki na Tanzania kwa upande wa wanawake.
“Unajua wenzetu wanajua mpira, na si kujua tu bali wanaujali mchezo wa soka kwa pande zote, wanawake na wanaume, wanachukulia kama kazi, hiyo si kwa shirikisho pekee bali hata nchi, wameuweka mchezo huo kama moja ya sehemu ya ajira.
“Uongozi kuanzia shirikisho wapo makini hawakai ofisini kusubiri kuletewa taarifa bali wanazungukia sehemu mbalimbali hata kutembelea timu hasa kama timu zinazojiandaa na mechi kubwa za kimataifa.
“Ni hivyo hivyo hata upande wa wachezaji huwa hawasubiri kusukumwa wanajituma wenyewe kwani wanatambua nini wanatakiwa kukifanya, wengi wanasoma, vyuoni kuna michezo inayoendeshwa kama ligi, wenzetu wanafundishwa kuanzia hatua ya mwanzo wanapokuwa watoto ndiyo maana wanajua na kuthamini soka lao, Uturuki kuna Ligi Tatu ya U-17, U-19 na ligi ya wakubwa ambayo ni Ligi Kuu,” anaeleza Mwasikili.
Beki huyo anasema kwa hapa Tanzania soka la wanawake halithaminiwi kwani hata hatua ya Ligi Kuu bado haijafikiwa jambo ambalo linakatisha tamaa na kuliomba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Chama cha Soka cha Wanawake (TWFA) kuanzisha Ligi Kuu ya Wanawake .
“Viongozi wetu watuombee hata udhamini ili iwepo Ligi Kuu ya Wanawake, wanawake tunaweza na tunapenda kuliko tofauti na wanavyofikiria mashabiki wa soka, hivyo tunaomba tusiishie kucheza ligi za chini kama Wilaya na Mkoa,” anasema.
Mwasikili alizungumzia pia juu ya mikataba baina ya wachezaji na klabu: “Tangu nimeanza kucheza soka katika timu ya Sayari Queens, nimeenda nje nimemaliza mkataba nimerudi kwenye timu yangu iliyonikuza sijawahi kupewa mkataba wa maandishi ni makubaliano tu.
“Mkataba wa maandishi ambao ni wa kwanza kwangu ni huo wa timu ya Uturuki, kule kila mchezaji ni lazima awe na mkataba na timu yake kitu ambacho hapa hakipo.
“Hapa mkataba wako unategemea na kiwango cha uchezaji wako ambapo pia unakuwa si maalumu hakuna kuandikishana yanakuwa ni makubaliano na makubaliano yenyewe yanaweza kuwa ni kulipiwa kodi ya nyuma ingawa napo mara nyingi haitimizwi,” anasema.
Mchezaji huyo anasema amewafaidi Wazungu wa Uturuki kwani mafanikio yake katika soka anayaona kwenye rasilimali zake japo ni haba; “Tangu nianze kucheza soka hapa nchini kwa kweli sijawahi kupata mafanikio yoyote, mafanikio nimeyapata nilipokwenda Uturuki kwani nilikuwa nalipwa vizuri mpaka nikafikia hatua ya kununua eneo la kujenga.
“Nimejenga nyumba yangu Kibada, Kigamboni jijini Dar es Salaam, nina maduka mawili ya nguo na maduka mawili ya kuuza vinywaji baridi, pia nina usafiri gari na pikipiki, kwa kweli ni matunda ambayo najivunia kutoka Uturuki.
“Nyumba yangu nimepangisha ila nina chumba changu kimoja ambacho huwa naenda mara moja moja kulala kwani bado nipo mikononi mwa wazazi wangu, naishi na mama huko Kigamboni, hataki nikae mbali na yeye.
“Nikiwa hapa faida ni kujulikana tu, unaweza kupanda daladala na wasikudai nauli kisa wanakufahamu au ukikaa sehemu unanunuliwa vitu au kinywaji, sasa hiyo ni hasara, kujulikana bila fedha si kuzuri,” anasema Mwasikili.
Mwasikili alieleza pia changamoto alizowahi kukumbana nazo.
“Nakumbuka ilikuwa mwaka 2004 nilivunjika mkono nikiwa na timu yangu ya Sayari, mwaka uliofuata niliitwa timu ya Taifa ‘Twiga Stars’ siku ya kwanza tu nilivunjika tena mkono ule ule, ni jambo ambalo sitalisahau sikuweza kucheza mpaka timu ilipotolewa kwenye mashindano.
“Lakini baadaye nilikuwa vizuri na changamoto nyingine ni majeruhi ya kawaida na kugombea namba ambapo mtu unatakiwa ujitume sana ili kocha aweze kukupanga kwa ajili ya kuisaidia timu,” anasema.
Ana malengo gani
“Mpaka sasa natazama nje zaidi, sifikirii kukaa hapa kwa kipindi kirefu kwani tayari nimeanza kufanya mipango ya kwenda kucheza soka la kulipwa Sweden ila nasubiri nirudi kwenye kiwango ambacho nakitaka.
“Mtu anaweza kukuona una kiwango kizuri lakini mimi naona bado, nataka nicheze kwanza hizi mechi za kimataifa ambazo nina uhakika zitarudisha kiwango changu hata rekodi yangu itakuwa nzuri ndipo niondoke,” anasema.
Mwaka 2006, Mwasikili alichaguliwa kuwa nahodha msaidizi lakini mwaka mmoja baadaye kocha wake alimteua kuwa nahodha mkuu cheo ambacho amedumu nacho mpaka sasa.

Mwanasipoti

No comments:

Post a Comment