Kundi la vijana 60, juzi walipora mwili wa marehemu Gabriel
Ngalele ukiwa unaombewa kwenye Kanisa la Tanzania Assemblies Of God
(TAG) eneo la Uyole jijini baada ya kuchoshwa na ibada ndefu ya
mchungaji.
Ibada hiyo ilikuwa ikiendeshwa na Mchungaji,
Edward Mtweve wa kanisa hilo ambaye alijikuta kwenye mazingira magumu
baada ya vijana hao wanaodaiwa kuwa ni madereva wa pikipiki kuvamia
madhabahu na kubeba sanduku lililokuwa na mwili wa marehemu.
Marehemu Ngatele alikuwa dereva wa pikipiki na
alifariki kwenye ajali iliyotokea eneo la Sae baada ya pikipiki yake
kuligonga lori lililoharibika katikati ya barabara. Katika ajali hiyo,
abiria pia alifariki.
Mwili wa marehemu ulipelekwa katika kanisa hilo,
na wakati mchungaji akiendesha ibada kulijitokeza kelele za hapa na pale
na kusababisha mchungaji kuomba utulivu mara kadhaa.
Lakini kelele nyingi zililipuka ghafla zikiwamo za
kulalamika kwamba ibada ilikuwa ndefu na hatimaye vijana wengi
walionekana wakiingia kwenye mlango na kuvamia madhabahu na kutoka na
mwili wa marehemu.
Baada ya kuuchukua mwili, vijana hao walikwenda
kwenye makaburi kuuzika wakati naye mchungaji akiendelea kuhubiri
waumini waliobaki ndani ya kanisa.
Mchungaji Mtweve alilazimika kwenda nyumbani baada
ya kumaliza ibada badala ya makaburini, huku vijana nao wakiendelea na
taratibu za mazishi kwa utaratibu uliosimamiwa na Mwenyekiti wa
waendesha pikipiki Mbeya, Vicent Mwashoma.
Mwendesha pikipiki aliyetajwa kwa jina la Bahati Mwasote alilazimika kuendesha ibada ya mazishi.
Mchungaji Edward Mtweve alipoulizwa kuhusu tukio hilo alisema alisikitishwa na kitendo cha kuvurugwa kwa ibada.
No comments:
Post a Comment