HAMU ya mashabiki wa soka Kenya kumuona kiungo Victor Wanyama
akiwatesa viungo wa Arsenal imezidi kuwa njia panda kutokana na balaa la
majeruhi linalomuandama.
Kiungo huyo wa Kenya anayeichezea Southampton leo
Jumanne alitarajiwa kuwa kibaruani kuikabili Arsenal katika mechi ya
Ligi Kuu England lakini hali yake bado si nzuri.
Mashabiki wengi wa soka nchini hapa hupenda
kumwangalia nyota huyo ambaye pia ni nahodha wa timu ya taifa ya Kenya,
Harambee Stars akiwajibika katika kikosi cha kwanza cha Southampton.
Kutokana na ushabiki wa Ligi Kuu England nchini
hapa, Wanyama anazidi kuongeza burudani awapo uwanjani jambo ambalo sasa
limeshindikana kwa kuwa nyota huyo ni mgonjwa.
Kocha Msaidizi wa Southampton, Jesus Perez
alibainisha kwamba ni mapema mno kwa mchezaji huyo kupona maumivu ya
mguu aliyoyapata katika mechi dhidi ya Aston Villa Desemba mwaka jana.
Awali kulikuwa na habari kwamba kiungo huyo
angekuwa amepona kwa wakati mwafaka na leo angevaa jezi ya Southampton
katika mechi hiyo ngumu dhidi ya Arsenal.
Kwa mujibu wa Perez huenda, Wanyama akawa nje ya uwanja kwa muda mrefu zaidi wakati akiendelea kujiuguza.
Hata hivyo Perez alisema kwamba mchezaji huyo
anafanya mazoezi ya kawaida lakini bado hayuko fiti kucheza mechi ya
ushindani na kwamba anachohitaji ni mazoezi maalum ya kumuweka katika
hali nzuri kushindana uwanjani.
Wanyama alijiunga na Southampton akitokea Celtic,
Julai waka jana kwa ada ya Pauni 12.5million na ameichezea timu hiyo
mechi 14 kabla ya kuumia.
No comments:
Post a Comment