Sunday, 19 January 2014

Waliofeli Kidato cha Pili kuendelea na Masomo

Wakati Watanzania wakisubiri matokeo ya kidato cha pili mwaka 2013, imebaini kuwa Serikali imetoa agizo kwamba wanafunzi wote waliofeli mtihani huo kuendelea na masomo ya kidato cha tatu, huku wakisoma mafunzo ya kurudia mtihani wa kidato cha pili.

Licha ya matokeo hayo kutotangazwa hadi sasa, imebainika kuwa waliofaulu mtihani huo uliofanywa Oktoba 7 hadi 21 mwaka jana ni asilimia 62 tu, asilimia 31 wakitakiwa kukariri (kurudia) kidato cha pili mwaka huu, huku asilimia saba wakishindwa mtihani huo kwa mara ya pili.

Jumla ya wanafunzi 531,457 walitajwa na Wizara ya Elimu mwaka jana kuwa watafanya mtihani huo.

Uamuzi huo wa Serikali ni tofauti na ule uliotolewa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa Novemba 4, mwaka 2012, kwamba kuanzia wakati huo mtihani wa kidato cha pili utakuwa ni wa mchujo na kwamba atakayefeli atatimuliwa.

Dk Kawambwa alisema matokeo ya mtihani wa kidato cha pili yatatumika kama kigezo cha kuchuja na kukariri kidato cha pili kwa watahiniwa watakaoshindwa kufikia wastani wa ufaulu wa alama 30.

Alisema mtahiniwa ataruhusiwa kukariri kidato cha pili mara moja tu na endapo mtahiniwa atashindwa mtihani kwa mara ya pili kwa mwaka utakaofuatia, itabidi aendelee na elimu ya sekondari nje ya mfumo rasmi.

Gazeti hili limeiona barua iliyoandikwa Januari 16 mwaka huu na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na kusainiwa na Katibu Mkuu wake, Profesa Sifuni Mchome, kwenda kwa wadau wa elimu nchini, wakiwamo maofisa elimu wa mikoa na Chama cha Wamiliki wa Vyuo na Shule Binafsi (TAMONGSCO).

Katika barua hiyo, wizara hiyo imewataka wadau hao kuhakikisha kuwa wanafunzi watakaofeli mtihani huo, wanaendelea na masomo ya kidato cha tatu.

“Matokeo ya kidato cha pili yamepokewa na kufanyiwa uchambuzi ili kupata taswira ya taifa. Taarifa ya matokeo hayo imebaini kuwa watahiniwa waliofanya mtihani na kufaulu ni sawa na asilimia 62 tu,” inaeleza sehemu ya barua hiyo na kuongeza;

“Hali hii inaonyesha kuwa asilimia 31 ya wanafunzi watatakiwa kukariri kidato cha pili, 2014. Wale walioshindwa kwa mara ya pili ambao ni asilimia saba wanatakiwa kuendelea na masomo nje ya mfumo rasmi.”

Barua hiyo inaeleza kuwa wanafunzi waliofaulu kwa wastani wa alama 20 na kuendelea waendelee na masomo ya kidato cha tatu mwaka 2014, wakati awali Serikali ilitoa tamko kuwa watakaoshindwa kufikisha alama 30 watatimuliwa.

“Wanafunzi waliofaulu kwa wastani wa alama 20 hadi 39 wapewe mafunzo rekebishi ‘Remedial class’ wakiwa kidato cha tatu,” inaeleza sehemu ya barua hiyo.


Inaeleza kuwa uamuzi huo unawahusu wote wakiwamo wale walioshindwa kwa mara ya pili, “Kwa maana hiyo hakuna mwanafunzi atakayerudishwa nyumbani.”

Mwisho barua hiyo imewataka wadau hao kuhakikisha kuwa inawapa taarifa mameneja na wamiliki wa shule na seminari ili kusimamia utekelezaji wa uamuzi kuhusu matokeo hayo.

Kauli ya wizara

Akitolea ufafanuzi suala hilo, Profesa Mchome alisema, “Suala la wizara kuagiza wanafunzi wote waliofeli kuendelea na masomo ya kidato cha tatu mimi sijalisikia, ninachojua ni kwamba wapo watakaorudia.”

Alisema kuwa tayari wizara imeshapeleka taarifa za matokeo hayo na uamuzi wa Serikali katika kila kanda nchini. “Kila shule ina taarifa hizo. Wapo wanafunzi watakaorudia.”

Akizungumza kuhusu matokeo ya kidato cha pili mwaka 2013 kutotoka mpaka sasa alisema, “Ninachofahamu ni kwamba matokeo ya kidato cha pili yameshawasilishwa katika kanda zote nchini.”

“Unajua matokeo ya kidato cha pili siyo kama matokeo ya darasa la saba, kidato cha nne na sita. Matokeo ya kidato cha pili ni kama mwendelezo wa tathmini ‘Continuous assessment’ kwa mwanafunzi, hutumika pia katika mtihani wa kidato cha nne.”

Alisema ndiyo maana matokeo hayo hupelekwa katika shule husika. “Baada ya kupelekwa katika shule husika, hapo ndipo inaweza kutolewa taarifa za matokeo hayo pamoja na ufafanuzi.”

Kwa nyakati tofauti gazeti hili lilimtafuta Dk Kawambwa na Naibu wake, Phillip Mulugo ili kutolea ufafanuzi suala hilo, lakini simu zao za mkononi zilikuwa zikiita bila majibu.

Msimamo wa TAMONGSCO

Alipotafutwa Katibu Mkuu wa Tamongsco, Benjamin Nkonya kueleza kama wanakubaliana na agizo hilo la Serikali alisema, “Inaonekana Serikali haiko tayari kutekeleza mkakati wake wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).”

“Kama wizara inalazimisha wanafunzi walio na ufaulu mdogo kuendelea na masomo katika mfumo wa vidato (formal education), lazima tutegemee kuona wanafunzi wakifanya vibaya katika mitihani ya kidato cha nne.”

Alisema kuwa asilimia 98 ya wanachama wa chama hicho ni Watanzania wazalendo kwamba hawapo tayari kutekeleza agizo la Serikali kwa sababu siyo la kizalendo na limetolewa kwa ajili ya kutimiza malengo ya kisiasa ya kujiongezea umaarufu wa muda mfupi, huku Watanzania wakiogelea kwenye dimbwi la umaskini unaotokana na ujinga.

“Wachache watakaosaliti msimamo huu watakuwa wamekubali kupoteza muda wa vijana wetu huku wakijua kwamba watafika kidato cha nne, kupata daraja sifuri na kuishia kuwa machangudoa, wauza dawa za kulevya, bangi, wizi na vitendo vingine vya uvunjifu wa sheria, kanuni na taratibu,” alisema.

Alisema ili kuwasaidia wanafunzi wanaoshindwa kuendelea na masomo yao; “Mwanafunzi ambaye ufaulu wake utakuwa chini ya asilimia 45 aondolewe katika mfumo wa elimu ya vidato (formal education) na kuingizwa katika mfumo wa elimu ya ufundi mchundo (TVET - Technical education and vocational education).”

Alisema wanachama wa Tamongsco wanamiliki vyuo 586 kati ya vyuo 750 vya ufundi mchundo (VETA) na wanamiliki vyuo 1975 kati ya vyuo 1988 vya ufundi stadi (technical institutes) ambavyo vinasimamiwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi Stadi (NACTE).

“Vyuo hivi vina uwezo wa kuchukua wanafunzi wote ambao wana ufaulu wa chini ya asilimia 45 kuwaendeleza hadi chuo kikuu. Kikwazo pekee kilichopo ni kwa Serikali kukubali kuchangia gharama za uendeshaji wake.”

“Kikwazo hiki kitaondoka endapo Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi itakubali kutekeleza sera, sheria na kanuni za ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP) partnership) kama ilivyopitishwa na Bunge mwaka 2010.

Kidato cha pili 2012

Katika mtihani huo mwaka 2012 wanafunzi 136,923 kati ya 386,271 waliofanya mtihani huo walifeli. Idadi ya waliofeli ilikuwa sawa na asilimia 35.5, wakiwamo wasichana 74,020 na wavulana 62,903, waliofaulu walikuwa wanafunzi 245.9,32.


CHANZO: Mwananchi

No comments:

Post a Comment