Wednesday, 22 January 2014

Kenya kuandaa Afcon 2019

HUENDA Kenya ikapata fursa ya kuandaa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2019 baada ya mamlaka ya soka Barani, CAF kuiuliza Shirikisho la Soka nchini FKF, kutoa uhakikisho wa kuungwa na serikali.
FKF walituma ombi la kutaka kupewa fursa ya kuandaa dimba hilo mwaka wa 2019 na sasa CAF inataka kupata uhakikisho kutoka kwa serikali ikiwa ipo tayari kuisaidia FKF kufanikisha mpango huo endapo ombi la Kenya litakubaliwa.
CAF yenye makao yake makuu jijini Cairo, Misri iliiandikia FKF barua ikitaka kupewa ufafanuzi na msimamo wa serikali kuhusu suala hilo kabla ya wao kufanya uamuzi.
Kupitia Naibu Mkurungezi wake, Khaled Nassar, CAF ilithibitisha kupokea ombi la Kenya la kutaka kupewa fursa hiyo ila ikalalamikia kukosa kupata uhakikisho wa serikali.
“Tumepokea ombi lenu kuhusu kupewa fursa ya kuwa wenyeji wa fainali za kuwania Kombe la Mataifa ya Afrika 2019. Ingawaje hatukupokea barua kutoka kwa serikali kutoa hakikisho pamoja na kuelezea ni mikakati ipi waliyonayo kuhusu hili kwa mujibu wa kaida zetu.
Hivyo basi tunawaomba mtujulishe ikiwa bado mna nia ya kufikiriwa katika ombi lenu kwa kuhakikisha mnatutumia stakabadhi tulizoziulizia,” CAF ilieleza. FKF walidokeza kwamba watajibu waraka huo.

Mwanasipoti

No comments:

Post a Comment