YANGA imetulia mjini Antalya, Uturuki ikipasha, na leo Jumatatu
mchana itacheza dhidi ya Simurq PIK inayoshiriki Ligi Kuu nchini
Azerbajain ikiwa ni mechi yake ya mwisho ya kirafiki nchini humo kabla
ya kurejea Tanzania Alhamisi wiki hii.
Mabosi wazito wa Yanga waliopewa jukumu la
kuiongoza klabu hiyo kwenye michuano ya kimataifa wamesisitiza kuwa
asilimia kubwa ya kazi hiyo imekamilika na wameshanasa mikanda mitano
yenye mbinu za Waarabu ambapo wanacheza mechi mbili kwa wakati mmoja.
Moja ya Wacomoro na ile ya Wamisri.
Yanga ambao wataingia kwenye Ligi ya Mabingwa
Afrika mwanzoni mwa mwezi ujao, wakianza na Komorozine ya Comoro jijini
Dar es Salaam na watarudiana wiki mbili baadaye mjini Moroni. Endapo
Yanga wakiwatoa Wacomoro hao, jambo ambalo si gumu watakwaana na Al Ahly
ya Misri kwenye mechi ya raundi ya kwanza.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Kimataifa ya
Yanga, Seif Ahmed ‘Seif Magari’ alisema kazi imeshaanza na walituma
mashushu wao kimya kimya nchini Comoro na Misri.
Seif alisema mara baada ya kukabidhiwa majukumu
hayo na baadaye kutoka kwa ratiba hiyo ya mechi za Ligi ya Mabingwa,
kazi kubwa ilianza kwa siri na alilazimika kutuma mashushushu wake
nchini Misri ambao walifanikiwa kupata mikanda ya mechi za Al Ahly
ambazo zote ni mechi za hivi karibuni na kwamba timu ikirudi kutoka
Uturuki atamkabidhi kocha Mholanzi Van der Pluijm mikanda hiyo.
Alisema mbali na ilichofanya kamati yake, Van der
Pluijm naye amewaambia anajua mambo mengi kuhusu Al Ahly ikiwemo mifumo,
staili zao za ushindi. Lakini wakati wakifanya hivyo wamehamishia
majeshi yao kwa Wacomoro na hawataidharau mechi hiyo.
“Nina watu wakunisaidia kutekeleza majukumu haya,
tumepata mikanda mitano ya mechi za Al Ahly, ipo mezani kwangu kwa sasa
na itatusaidia, tutamkabidhi kocha na hata yeye kocha ameshafanya kazi
moja ya kupata mifumo yote ambayo inatumiwa na Al Ahly,
ametutahadharisha na fitna za hawa Waarabu kwa sababu aliwahi kucheza
nao mwaka jana,”alisema Seif.
“Moja ya jambo baya walilowahi kufanyiwa akiwa na
timu yake ya Berekum Chelsea ya Ghana ni kupewa kadi nyekundu kwa
mchezaji wao mmoja mapema sana, ametuonya tuwe makini sana. Watu
wanaweza kuona kama tumewadharau hawa Wacomoro lakini hapana nao tupo
katika hatua za mwisho kupata mikanda yao, kuna watu tumeshawapa hiyo
kazi wapo kazini sasa.
“Wakikamilisha watawasilisha hiyo mikanda
haraka,”alisema Seif kwa kujiamini huku akisisitiza kuwa vijana wake kwa
sasa wapo nchini Comoro kwenye hatua za mwisho kabisa za kukamilisha
majukumu yao.
Wakati Yanga wakifanya kazi hiyo, Shirikisho la
Soka Afrika (CAF) limetoa majina ya waamuzi watakaochezesha mechi hiyo
ya kwanza ya Yanga dhidi ya Komorozine waamuzi hao ni kutoka Somalia.
Mwamuzi wa kati ni Hassan Mohamed Hagi wakati wasaidizi wake ni Hamza
Hagi Abdi, Bashir Abdi Suleiman na Bashir Olab. Kamishna wa mechi hiyo
atakuwa Eugene Musoke kutoka Uganda.
Mwanaspoti
Mwanaspoti
No comments:
Post a Comment