Wednesday, 29 January 2014

RWANDA YAZIDI KUMCHOKAZA JAKAYA KIKWETE



BUSARA ya Rais Jakaya Kikwete juu ya kuitaka Serikali ya Rwanda kukaa kwenye meza ya mazungumzo na waasi wa FDLR, imeendelea kutafsiriwa vibaya na baadhi ya wakubwa wa nchi hiyo, ambapo sasa wameanza kumchokonoa kwenye baadhi ya vyombo vya habari, kwa kudai kuwa amekutana kwa siri jijini Dar es Salaam na waasi hao. 

Gazeti la News of Rwanda ambalo linatajwa kuwa mshirika mkubwa wa Serikali ya nchi hiyo, katika toleo lake la Jumapili iliyopita, liliandika kuwa Rais Kikwete amekutana na waanzilishi wa chama cha upinzani nchini humo cha Rwanda National Congress (RNC) na makamanda waandamizi wa waasi wa FDLR.

Habari iliyoandikwa na gazeti hilo, imebainisha kuwa kikao hicho cha Rais Kikwete na watu hao kilifanyika kwenye makazi binafsi ya Rais Kikwete.

Gazeti hilo lilidai kuwa limepata taarifa hizo kutoka kwenye vyanzo vyake vya habari vilivyopo nchini Tanzania, ambapo viliwaeleza kuwa ujumbe huo uliwasili, jijini Dar es Salaam Alhamisi ya wiki iliyopita.

Wameandika kuwa viongozi wa RNC waliokutana na Rais Kikwete ni Mratibu wa chama hicho, Dk. Theogene Rudasingwa na mshauri wake, Condo Gervais.

Katika kikao hicho, News of Rwanda lilidai kuwa kundi la waasi wa FDLR, liliwakilishwa na Katibu Mtendaji wake, Luteni Kanali Wilson Irategeka na Kanali Hamadi ambaye ni kamanda wa operesheni.

Luteni Kanali Irategeka kwa sasa anatajwa kuwa ndiye nembo ya waasi wa Rwanda wa kundi la FDLR na mara kwa mara amekuwa akionekana kwenye mahojiano na vyombo vya habari. 

News of Rwanda liliendelea kuandika kuwa, majina hayo anayotumia Luteni Kanali Irategeka si yake na kwamba jina lake kamili ni Ndagijimana.

Viongozi hao wa FDLR wote wanaishi Washington, nchini Marekani na kwamba wanasafiri kwa kutumia hati za kusafiria za Tanzania.

Hata hivyo, News of Rwanda wameshindwa kuthibitisha madai yao ya pasi za kusafiria za waasi hao kama zimetolewa na Serikali ya Tanzania, au zilipatikana kwa mlango wa nyuma.

Aidha gazeti hili lilikwenda mbali zaidi kwa kudai kuwa Januari 19, mwaka huu, Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo, Faustin Twagiramungu alikuwa Tanzania kwa shughuli kama iliyofanywa na waasi wa FDLR.

Walidai kuwa hata hivyo aliondoka Tanzania Alhamisi ya wiki iliyopita, kuelekea Lyon, nchini Ufaransa ambako alikuwa aongoze kikao cha kundi lake la kisiasa la RDI na Rwanda RWIZA.

Limedai, Twagiramungu aliondoka kabla ya timu ya RNC haijawasili Dar es Salaam, ingawa Twagiramungu pia alipaswa kuwa pamoja na RNC na FDLR.

News of Rwanda halikuweza kubainisha kilichopelekea Twagiramungu kuamua kukaa mbali na wenzake hao, ingawa walidai kwamba Waziri Mkuu huyo wa zamani hataki kuingia tena katika ndoa ya kisiasa na kundi linalohusisha waanzilishi wanne wa RNC.

Twagiramungu ndiye Waziri Mkuu wa kwanza kushika wadhifa huo mara baada ya kumalizika kwa mauaji ya kimbari, ambapo alishika wadhifa huo kwa kipindi cha mwaka mmoja na baadaye kujiuzulu.

Limebainisha kuwa, Twagiramungu amekuwa na uhusiano mbovu na Dk. Rudasingwa na Kayumba Nyamwasa kutokana na kuwa sababu ya yeye kushindwa kutekeleza majukumu yake na kuamua kuachia ngazi.

Wawili hao wamedaiwa kuwa walikuwa maofisa waandamizi katika nyadhifa kubwa kisiasa na kijeshi nchini Rwanda.

News of Rwanda limebainisha kuwa, Twagiramungu na makundi mengine ya waasi ya Rwanda, yameapa kutoingia katika ushirika wa kisiasa na watu waliokuwa karibu na Serikali, baada ya kutofautiana na utawala wa Rais Kagame. 

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari, si mara ya kwanza kwa wawakilishi wa RNC wanaomwakilisha Kayumba Nyamwasa, kukutana na waasi wa FDLR. 

Gazeti hili limezidisha chokochoko kwa kudai kuwa Desemba 20, 2013, Luteni Kanali Wilson Irategeka na Kanali Hamadi walisafiri wakitumia hati ya kusafiria za Tanzania kwenda Msumbiji kwa mazungumzo na wajumbe wa RNC, na kwamba Tanzania imekuwa ikitoa hifadhi kwa waasi wa FDLR. 

Katikati ya mwaka jana, Naibu Kamanda wa FDLR, Jenerali Stanislas Nzeyimana, maarufu kama Izabayo Bigaruka, alitangazwa kuwa yupo Tanzania. Lakini wiki kadhaa baadaye, taarifa ziliibuka kuwa ametoweka na kuzua maswali ya sababu za uwepo wake Tanzania.

Katika kuhitimisha chokochoko zao, News of Rwanda liliandika kuwa nchini Tanzania, upinzani haufurahishwi na mwelekeo wa Rais Jakaya Kikwete kuwabeba FDLR, na kwamba Agosti mwaka jana, CHADEMA, ambacho ni chama kikuu cha upinzani Tanzania, kilimtuhumu Rais Kikwete kwa kutokuwa tayari kukutana na wapinzani nyumbani na kuingilia mambo ya ndani ya Rwanda.

“Hakuna dhati yoyote ndani ya taarifa ya Rais Kikwete kuwa Rwanda inapaswa kuzungumza na kundi la wanamgambo wa FDLR, ambalo limekuwapo katika misitu ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo tangu 1994,” walimnukuu Dk. Willbrod Slaa, ambaye ni Katibu Mkuu wa CHADEMA

Katika kuhalalisha kile walichokiandika, News of Rwanda liliendelea kumnukuu Dk. Slaa kuwa: “Iweje Rais Kikwete hayuko tayari kujadiliana na upinzani nyumbani na kwamba, Rais Kikwete hajachukua hatua zozote kuhusu wauaji wa mwandishi, Daudi Mwangosi, na kwamba alimshauri (Kikwete) kuchukua hatua za kumwajibisha Kamanda wa Polisi Mkoa Iringa, Michael Kamuhanda badala yake alimpandisha cheo,” walihitimisha nukuu yao.
-Mtanzania

No comments:

Post a Comment