Aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja
ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba,
Sheria na Utawala Uchaguzi. Uteuzi huo ulitangazwa jana baada ya kamati
mbalimbali za Bunge kufanya uchaguzi kujaza nafasi tisa zilizoachwa wazi
na wenyeviti na wajumbe wa kamati hizo ambao wameteuliwa na Rais Jakaya
Kikwete katika Baraza la Mawaziri.
Mbali ya Ngeleja ambaye anachukua nafasi ya Pindi Chana aliyeteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto.
Kabla ya hapo, Ngeleja ambaye ni Mbunge wa
Sengerema (CCM) alikuwa Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, nafasi ambayo
sasa imechukuliwa na Mbunge wa Karagwe (CCM), Gosbert Blandes.
Pia Mbunge wa Mchinga (CCM), Said Mtanda
amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Jamii kujaza
nafasi ya Jenister Mhagama aliyeteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Elimu na
Mafunzo ya Ufundi.
Mtanda pia alikuwa Makamu mwenyekiti wa kamati
hiyo kabla ya uchaguzi wa jana na nafasi yake imechukuliwa na Mbunge wa
Mbinga Magharibi (CCM), John Komba.Mbunge wa Meatu (CCM), Luhaga Mpina
amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi, Viwanda na Biashara
nafasi ambayo ilikuwa ikishikiliwa na Mahmoud Mgimwa aliyeteuliwa kuwa
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii. Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo
anaendelea kuwa Mbunge wa Mkinga (CCM), Dunstan Kitandula.
Wazungumza
Akizungumzia uteuzi huo, Ngeleja alisema changamoto kubwa anavyokabiliwa nayo baada ya kuchaguliwa ni mchakato wa Katiba Mpya.
Alisema kamati yake ni mdau mkubwa wa mchakato huo
na kwamba akishirikiana na wajumbe wake, wamepania kuona ikipatikana
Katiba inayowakilisha masilahi ya watu wote.
“Hatutapenda kuona wanasiasa wanakuwa juu ya
mchakato wa Katiba, tutahakikisha mawazo ya makundi yote yanaheshimiwa
wakati wa mchakato huu,” alisema. Akizungumza baada ya kuteuliwa, Mtanda
alisema: “Kazi kubwa iliyopo mbele yetu ni kupigania pensheni ya wazee,
kukabiliana na changamoto za ajira kwa vijana pamoja na kuhakikisha
kuwa Muswada wa Sheria ya Vyombo vya Habari unafikishwa bungeni na
kujadiliwa.” Uchaguzi wa kamati nyingine ambazo wenyeviti na makamu wake
wameteuliwa kuwa mawaziri utaendelea leo.
Pia Spika wa Bunge anatarajiwa kuwarejesha katika
kamati mbalimbali mawaziri tisa ambao wameachwa na Rais Kikwete katika
Baraza lake la Mawaziri.
Mawaziri hao ni wale watano walioachwa baada ya
Rais Kikwete kufanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri na wengine wanne
ambao alitengua uteuzi wao Desemba 20 mwaka jana baada ya wizara zao
kutajwa kushindwa kusimamia Operesheni Tokomeza Ujangili.
Kwa mujibu wa kanuni za Bunge, Mbunge akiteuliwa
kuwa waziri moja kwa moja anakuwa amepoteza sifa ya kuwa mjumbe wa
kamati yoyote ya Bunge.
No comments:
Post a Comment