Hukumu iliyokaziwa na Mahakama ya Rufaa, Dar es Salaam, juzi (Alhamisi), ikipigilia msumari adhabu ya kifungo cha maisha jela dhidi ya mwanamuzi mkongwe nchini, Nguza Viking ‘Babu Seya’ na mwanaye, Johnson Nguza ‘Papii Kocha’, imesababisha maumivu makali kwa wahusika.
Uthibitisho wa hilo unatokana na kauli ya Babu Seya, aliyoitamka mahakamani akimnong’oneza Papii Kocha, akisema: “Kweli hii dunia haina huruma, hukumu hii imeniuma sana kuliko zote ambazo zimetangulia.”
Akizungumza kwa upole kwa sauti ya majonzi, huku sura yake ikionesha dhahiri kutokuwa na furaha, Babu Seya aliendelea: “Kinachoniuma zaidi ni wewe, nakusikitikia sana, wewe ni kijana mdogo ambaye ulipaswa kuwepo uraiani ukitimiza ndoto zako na ukiisadia nchi yako.
...Akiwa katika huzuni na majonzi makubwa.
“Ndoto zako zimeishia hapa. Tumejitahidi sana kukwepa hiki kifungo lakini imeshindikana, wewe unajua.”Hata hivyo, wakati akitoka nje ya ukumbi wa mahakama, Babu Seya alimweleza mwandishi wetu: “Hili jambo sijalifanya, nitaendelea kupambana mpaka mwisho.”
NI HUKUMU YA MWISHO
Msajili Mwandamizi wa Mahakama, Zahra Mruma, akisoma hukumu hiyo alisema: “Ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka ambao ni Jamhuri, umeendelea kuwa na nguvu, kwa hiyo vipengele vya utetezi vilivyowasilishwa na mawakili wa utetezi vimekosa nguvu ya kutengua hukumu ya awali.”
...Ndugu na jamaa wakiangua kilio baada ya hukumu.
Zahra, alisoma hukumu hiyo kwa niaba ya jopo la majaji watatu ambao
waliipitia upya hukumu hiyo, baada ya mawakili wa utetezi, Mabere
Marando na Gabriel Mjele, kuomba Mahakama ya Rufaa ifanye mapitio ya
mwisho, baada ya kutokuzikubali zote zilizotangulia.Mawakili wa upande wa utetezi, walitaka mapitio hayo yafanyike kwa hoja kwamba haiingii akilini kwa Babu Seya na mwanaye kushiriki tendo la mapenzi kwa pamoja, tena kwenye nyumba wanayoishi.
Hoja hiyo ilishibishwa na maelezo kuwa Babu Seya na Papii ni Waafrika, kwa hiyo kitamaduni haiwezekani kushiriki mapenzi kwa pamoja.
Utetezi mwingine ni kuwa nyumba ya tukio ni ya kifamilia, kwa hiyo isingekuwa rahisi kwa tendo husika kutendeka, maana wengi wangekuwa wanashuhudia.
KESI YA MSINGI
Babu Seya na Papii, walishtakiwa na baadaye kukutwa na hatia ya kuwabaka, kuwalawiti na kuwaambukiza Virusi Vya Ukimwi, watoto nane, wenye umri wa kati ya miaka saba na sita.
Mahakama ilielezwa kuwa Babu Seya alikuwa akiwaita watoto hao na kuwanunulia pipi kisha kuwaingiza ndani ambako waliwaingilia kwa zamu na baada ya kitendo, waliwapa mgao wa kati ya shilingi 100 na 150.
Kesi hiyo iliwasilishwa mahakamani kwa mara ya kwanza mwaka 2003 na mwaka 2004, hukumu ilitolewa, ikiwatia hatiani Babu Seya na wanaye watatu na kuwahukumu kwenda jela maisha.
Watoto wengine wawili wa Babu Seya, waliokuwemo kwenye kesi hiyo ni Francis Nguza na Nguza Mbangu ‘Nguza Mashine’ aliyekuwa mpiga drum wa Bendi ya FM Academia, mpaka wakati anaingizwa kwenye mashtaka.
Mwaka 2005, rufaa ya kwanza ilisomwa ambayo ilikazia hukumu ya awali lakini Februari 2010, Mbangu na Francis waliachiwa huru baada ya kuonekana hawana hatia, huku Babu Seya na Papii, ikipitishwa na Mahakama ya Rufaa kwamba waendelee na kifungo cha maisha jela.
MAJAJI WALIVYOTOA HUKUMU
Zahra, alisema jopo la majaji watatu, Nathalia Kimaro, Salum Masati na Mbarouk Salim Mbarouk, lilichambua hoja za utetezi na kuona hazina nguvu, kwa hiyo wakajiridhisha kuwa Babu Seya na Papii, wanastahili kuendelea na adhabu ya kifungo cha maisha jela.
Hukumu hiyo, ilikuwa ni ya rufaa ya nne, lakini imeshindikana kwa kuwaondoa Babu Seya kwenye kifungo.
MAWAKILI WASALIMU AMRI
Mmoja wa mawakili wa utetezi, Mjele, alisema kuwa hukumu hiyo ndiyo ya mwisho na kwamba wao hawana njia nyingine ya kukata rufaa kisheria.
“Hatuna njia nyingine, hapa ndiyo mwisho,” alisema Mjele na kuongeza: “Labda tusubiri msamaha wa rais kwa sababu ni yeye pekee mwenye mamlaka ya kutengua hii adhabu.”
RAIS AZIDI KUTUPIWA MZIGO
Watu kadhaa waliohudhuria mahakamani juzi, waliungana na Wakili Mjele kwamba kesi hiyo iachwe mikononi mwa rais kwa sababu ndiye mwenye nafasi ya kufanya lolote katika kesi hiyo kama anavyoruhusiwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Mahakama imefanya kazi yake, mawakili wa utetezi wamejitahidi lakini imeshindikana, sasa hatutakiwi kuijadili sana hukumu, badala yake tumuachie rais kwa sababu ndiye mwenye mamlaka,” alisema Fredrick Mwaluwanda wa Kinyerezi.
Mosha Kabogo alisema: “Katika hukumu hii, kila mmoja anaweza kuwa na hisia zake, jambo la msingi ni kumuacha rais afanye anachoona kinafaa. Uzuri ni kwamba siyo rais wa sasa peke yake, kwani hata ye yote anayekuja, anaweza kutumia mamlaka yake kikatiba kuwaachia huru au kuwapunguzia adhabu.”
WANAMUZIKI WAANDAA UJUMBE KWA RAIS
Mwanamuziki wa Bongo Fleva, Abdul Sykes ‘Dully Sykes’, alisema mahakamani hapo kuwa anakusudia kuitisha kongamano la wanamuziki halafu watafanya mkutano na waandishi wa habari kumuomba rais awaachie huru Babu Seya na Papii.
“Hili suala linauma sana, hatuwezi kukaa kimya tukiwaacha wanamuziki wetu nyota wakienda na maji. Lazima tufanye kitu na tutakachofanya ni kujikusanya na kuandaa mkutano wa waandishi wa habari ambao tutautumia kutuma ujumbe kwa mheshimiwa rais,” alisema Dully.
PAPII NI WA KUMJADILI KIDOGO
Papii Kocha, wakati alipoingia kwenye mashtaka hayo, alikuwa ni kijana mdogo ambaye nyota yake kwenye muziki ilikuwa inang’ara kwa kiwango cha juu sana nchini Tanzania.
Alifanya vizuri sana akiwa na Bendi ya FM Academia na Tot Plus kabla ya kutoka na albamu yake binafsi iliyokuwa na nyimbo nyingi kama vile Salima, Fanta na Seya ambayo uliimbwa mithili ya wimbo wa taifa.
Alitabiriwa kwamba angeweza kuendelea kufanya vizuri kutokana na uwezo aliokuwa nao lakini nyota yake ilizimwa na kesi hiyo.
Kwa upande wa Babu Seya, ni nguli aliyejenga jina na heshima kubwa nchini kupitia muziki wake, huku akipigiwa mfano kama mpiga solo bora kabisa, lakini historia yake imehitimishwa kwa kifungo cha maisha jela.
No comments:
Post a Comment