USAJILI wa dirisha dogo utaanza rasmi Ijumaa ijayo. Yanga
imedhamiria kuongeza wachezaji watatu kwa nafasi ya straika, kiungo
mshambuliaji na beki wa kati.
Hata hivyo Yanga wameweka wazi kwamba timu hiyo
itaweka kambi nje ya nchi kujiandaa na mzunguko wa pili na Ligi ya
Mabingwa Afrika.
Kambi hiyo, itawekwa katika nchi mojawapo ya
Afrika na kama mpango wao utakwenda sawa zaidi watarudi Ulaya kama
walivyofanya mwaka jana walipoweka kambi Uturuki.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano na Usajili wa
Yanga, Abdallah Bin Kleb aliliambia Mwanaspoti kuwa:”Tunataka
kujiimarisha kwa kila kitu ili Yanga iwe timu bora si kwa Tanzania tu,
bali Afrika kwa ujumla. Kwa hivyo hata wachezaji, watakaoongezwa ni
wenye kiwango bora. Tumeshaanza kufanya marekebisho mbalimbali ambayo
mwalimu kabla ya kuondoka alituagiza tuyafanyie kazi kwa kuongeza baadhi
ya wachezaji.”
“Katika usajili wetu wa dirisha dogo, tutasajili
wachezaji watatu na kama wataongezeka, hawatazidi wanne baada ya Kaseja
(Juma), tunaowahitaji kwa sasa ni straika, kiungo mshambuliaji na beki
wa kati, yeyote atakayekuwa mzuri wa kutufaa tutamsajili.
“Tuna nafasi moja ya mchezaji wa kigeni na huyu
ndiye anayeweza kuwa straika au kiungo mshambuliaji na tayari tuna
mitego yetu mbalimbali tumeshaiweka kwa ajili ya kukamilisha suala
hili,”alisema Bin Kleb na kufafanua sababu ya kumsajili Kaseja kuwa ni
uzoefu wake ili awasaidie kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
Akizungumzia kambi ya timu, Bin Kleb alisema:
“Mpango wetu ni kuweka kambi nje ya nchi. Inaweza kuwa nje ya Afrika
Mashariki kwa sababu bado tunaendelea na mipango ya kupata mahali pazuri
ambapo patakuwa na vifaa na mazingira mazuri.”
“Ndani ya wiki hii, mpango mzima utakamilika
kufahamu ni lini na mahali gani tutakwenda, kinachotuchanganya kwa sasa
ni haya mashindano ya Chalenji,”alifafanua.
Chalenji inaanza Novemba 27 hadi Desemba 12 nchini
Kenya ikihusisha Zanzibar Heroes, Uganda, Burundi, Rwanda na
Kilimanjaro Stars ambazo zote zina wachezaji kutoka Yanga.
No comments:
Post a Comment