MUDA halisi unaohisiwa atakuwa nje ya uwanja ni miezi sita,
lakini itategemea maendeleo yake baada ya kufanyiwa upasuaji na
watakachosema madaktari wa Real Madrid.
Lakini, ukubwa wa tatizo linalomkabili imeelezwa
kwamba itakuwa maajabu kumwona kiungo Mjerumani Sami Khedira akirudi
tena uwanjani msimu huu baada ya kuumia goti katika mechi ya kirafiki
dhidi ya Italia iliyofanyika Ijumaa iliyopita.
Na kwa kipindi chote hicho Real Madrid itacheza
bila ya huduma ya mchezaji wao huyo, aliyeumia akiitumikia Ujerumani
kwenye mechi za kirafiki za Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa)
lakini klabu hiyo italipwa fidia ya pesa. Kuanzia siku 29 ya mchezaji
huyo kukaa nje, Fifa itawajibika kulipa Pauni 20,548 kwa siku
atakayokuwa nje mchezaji husika ikiwa ni sehemu ya fidia kutokana na
kuiingizia gharama klabu kwa mchezaji huyo kuumia kwenye mechi za
kimataifa.
Kwa utaratibu huo, Real Madrid itaanza kupokea
pesa za Fifa kuanzia Desemba 14 mwaka huu na hilo litaendelea hadi hapo
madaktari watakapothibitisha kwamba mchezaji huyo yupo fiti kwa ajili ya
kurejea uwanjani.
Mwaka jana Real Madrid ilipokea jumla ya Pauni 1.1
Milioni kutokana na majeruhi ya Mbrazili Marcelo aliyeumia akiitumikia
Brazil.
No comments:
Post a Comment