KIPA wa Gor Mahia ya Kenya Ivo Mapunda amewaambia Simba kuwa Bobby Williamson ni bonge la kocha.
Mapunda, ambaye ameitwa katika kikosi cha Taifa
Stars amesema Simba hawatafanya makosa kumchukua kocha huyo kwani ni
kipenzi cha wachezaji na ana vitu vya ziada kiufundi.
“Kama Simba watamchukua Bobby watakuwa wamelamba
dume, ni kocha mzuri, ana vitu ambavyo makocha wengi wamevikosa, kikubwa
ninachosema ni kuwa Bobby anapenda kuwa karibu sana na wachezaji,”
alisema Mapunda.
“Unajua kocha yeyote ili uwe mzuri na ufanikiwe
uwe karibu na wachezaji, ujue matatizo yao na kuyatatua, uwafanye
marafiki, na ndivyo anavyofanya Bobby ndio maana anafanikiwa tofauti na
makocha wengine wanaweka mipaka kwa wachezaji wao,” alifafanua kipa huyo
wa zamani wa Prisons na Yanga.
“Gor Mahia imekaa miaka 18 bila kutwaa ubingwa,
lakini Bobby alipoajiriwa kuinoa tu akatuita sisi na timu imechukua
ubingwa baada ya miaka hiyo yote, ni wazi ni kocha ambaye anajua nini
anafanya,”alisema.
Kauli ya Mapunda imekuja wakati Simba ipo katika
mabishano makubwa ya kubadilisha benchi lake la ufundi huku Mwenyekiti
Ismail Aden Rage akiwa upande wa makocha wa sasa Abdallah Kibadeni
‘King’ na Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ huku wengine wakitaka makocha hao
wabadilishwe.
Boby Williamson (52), ni straika wa zamani wa West Bromwich Albion na katika mechi 53 aliyoichezea timu hiyo alifunga mabao 11.
Williamson, ambaye alikuwa kocha wa timu ya taifa
ya Uganda na kuipa ubingwa wa Kombe la Chalenji mara nne, ni kocha
anayesifika kutokana na kufundisha soka la kisasa kwa timu kushambulia
na kukaba kwa pamoja.
Mwanaspoti
Mwanaspoti
No comments:
Post a Comment