NAIBU Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January
Makamba amemshauri Mwenyekiti wa Yanga, Yusuph Manji kuachana na wadhifa
huo na kugeukia ukurugenzi wa soka la vijana.
Makamba, ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye halfa
ya utoaji Tuzo ya Mwanasoka Bora wa Tanzania 2012/13 iliyofanyika kwenye
Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam Ijumaa iliyopita alisema kuwa
soka la Tanzania haliwezi kufika mbali bila kuwapo na utaratibu mzuri wa
kuwekeza kwenye soka la vijana kuanzia miaka tisa.
“Naamini hii ndiyo sehemu ambayo tunakosea, kwa
maana hiyo kama ningekuwa Manji (Yusuph) basi ningeachana na uenyekiti
na kuomba ukurugenzi wa timu ya vijana, ifike mahali kuwe na utaratibu
kwa kila klabu inayoshiriki Ligi Kuu kuwa na akademi yake, tofauti na
hapo nafikiri tutaishia kupiga kelele pasipo mabadiliko yoyote,”
alisema.
Makamba ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli
aliipongeza klabu ya Azam kwa jitihada zake za kuanzisha Akademi kwa
ajili ya kulea na kukuza vipaji vya soka la vijana.
“Azam wameonyesha hilo, nawapongeza na iwe mfano kwa klabu nyingine kukomboa soka letu,” alisema.
Makamba pia aliimwagia sifa Kampuni ya Mwananchi
Communications Limited (MCL) ambayo inachapisha magazeti ya Mwananchi,
Mwanaspoti na The Citizen kwa kuanzisha Tuzo ya Mwanasoka Bora.
“Nawapongeza MCL pamoja na gazeti la Mwanaspoti
kwamba haliishii kuripoti habari bali hata kusaidia kuinua soka la nchi
yetu. Ni kitu kizuri mmekianzisha, naamini kitawapa changamoto mpya
vijana wetu na kusaidia kuinua soka letu,” alisema Makamba.
No comments:
Post a Comment