Friday, 15 November 2013

CHANGUDOA AKIRI KUCHOSHWA NA BIASHARA YA KUUZA MWILI WAKE, AELEZEA KWA UCHUNGU UGUMU WA BIASHARA HIYO.!!

INAWEZEKANA umeshalizwa na mengi, umesikitishwa na vingi lakini stori ya dada Aziza Athumani (21), anayefanya biashara ya kuuza mwili wake, inatia uchungu sana

Aziza anayefanya biashara ya kujiuza jijini Dar es Salaam kwa sasa ni mgonjwa lakini analazimika kuendelea na biashara hiyo ili aweze kujikimu.

Sasa, hebu fuatilia mahojiano yetu na Aziza.

Ijumaa: Hebu tuambie...ni nini hasa kilikusukuma kuingia kwenye biashara hii haramu?

Aziza: Maisha kaka yangu, maisha. Nilizaliwa Mtwara miaka 21 iliyopita. Niliishi na mama na wadogo zangu. Baba yangu anaishi hapa Dar. Bahati mbaya,  baadaye mama alifariki dunia. Hapo ndipo maisha yalipoanza kuwa magumu.

Ijumaa: Kwa hiyo shughuli ya kujiuza ulianza hukohuko Mtwara?

Aziza: Hapana. Maisha yalivyokuwa magumu baada ya mama kufariki, niliamua kuja Dar kutafuta maisha. Nilifikia kwenye baa moja iliyopo Sinza, nakumbuka ilikuwa mwaka 2010, nikiwa na miaka 17. Kipato kilikuwa kidogo sana lakini wateja walikuwa wakiniachia chenji ndogondogo.

Ijumaa: Kwa siku ulikuwa unaweza kuingiza shilingi ngapi?

Aziza: Hadi 10,000 nilikuwa nafikisha, wakati mwingine inazidi kidogo. Tatizo wanaume wa baa siyo wastaarabu. Wakilewa wanaanza kukushikashika. Mimi nilikuwa mdogo kwa hiyo nilivyokataa, nilifokewa na meneja. Nikawa nawaachia.

Siku moja, mteja mmoja akanitaka, nikakataa. Ikawa kama wameambiana. Karibu wote waliokuwa wakiniachia chenji wakanitongoza, wote nikawakataa, kuanzia hapo wakawa hawaniachii chenji tena. Maisha yakabadilika.

Ijumaa: Yakawaje?

Aziza: Nikawa sina fedha za kutosha kujikimu mimi na wadogo zangu. Wakati mwingine nilikuwa nalala mwenyewe geto (chumbani), wenzangu wote waliondoka na wateja (kulala nao kwa kujiuza). Nikiwaomba pesa, wananicheka, wakaniambia na mimi nitoke. Nikajaribu...kumbe nilikuwa naingia kwenye moto (analia)...nikajikuta nimezoea mchezo wa kujiuza.

Ijumaa: Usilie tafadhali, tulia. Baada ya hapo ikawaje sasa?

Aziza: Niliona biashara ya kujiuza inalipa zaidi kwa hiyo nikaamua kuachana na baa na kujikita moja kwa moja kwenye uchangudoa. Siamini kama mimi ni changudoa lakini sitaki kabisa hii kazi, ni shida tu kaka.

Ijumaa: Pole sana...vipi kuhusu baba yako? Halafu huo mguu una tatizo gani? Pia unaweza kueleza kidogo kuhusu elimu yako?

Aziza: (analia sana – zilipita dakika tano akiendelea kulia. Juhudi za kumbembeleza zilizaa matunda baada ya muda huo).

Ijumaa: Najua inauma sana. Jipe moyo. Unaweza kuendelea sasa!

Aziza: (anafuta machozi) Huyo baba...mzee Athumani ndiyo chanzo cha matatizo haya yote! Mimi sijasoma, niliishia darasa la saba tu. Lakini nikasema nitajitahidi angalau niwasomeshe wadogo zangu ndiyo maana nikaja mjini na kujikuta nimeishia kwenye biashara ya kujiuza.

Kuna tukio ambalo siwezi kulisahau. Ilikuwa Jumamosi, saa 9 usiku, mwezi wa saba, mwaka 2011. Mimi na rafiki yangu Asha tulikuwa tumetoka kujiuza Kinondoni. Tulikodisha pikipiki moja, tukapanda kwa mtindo wa mshikaki. Kwa bahati mbaya, tulipofika Magomeni tukapata ajali mbaya. Asha na dereva walikufa palepale...Mungu amrehemu rafiki yangu Asha (analia tena...).

Nikapelekwa Muhimbili, Kitengo cha Mifupa (MOI), nikalazwa kwa siku kadhaa. Mguu wangu ulikuwa umeharibika sana na hivi unavyoona nina vyuma. Niliporuhusiwa hospitalini, nikaenda kwa baba yangu mzee Athumani, Tandika. Cha ajabu, aliponiona nina magongo, akanifukuza akisema, eti mimi siyo mwanaye. Nililia sana, lakini kwa sababu nilikuwa na akiba kidogo nikaamua kurudi nyumbani kwangu Tandale nilipopanga chumba kimoja.

Pesa ilivyoisha, nikalazimika kurudi tena mtaani kujiuza na hii hali yangu ya magongo. Maisha haya! Sijui kwa nini inakuwa hivi jamani!

Ijumaa: Pole sana dada. Hebu tuambie...unakutana na changamoto gani katika kazi yako?

Aziza: Nyingi lakini kubwa ambayo sitaweza kuisahau ni kubakwa na wanaume watatu kwa mpigo, tena nikiwa na magongo yangu. Iliniuma sana. Wanadamu wana roho mbaya sana. Nilikutana na kaka mmoja, tukakubaliana angenipa shilingi 5,000 kwa muda mfupi.

Akasema, hana pesa ya kwenda gesti hivyo tukaenda kwenye Uwanja wa Urafiki, Shekilango. Nikashangaa nimekutana na wenzake wawili, nilipokataa, walinitolea kisu, ikabidi nikubali tu. Niliumia sana siku hiyo (analia – waandishi wanambembeleza).

Tukio lingine ni pale nilipokutana na mwanaume mmoja mwenye asili ya India, akanidanganya na kuniambia nimzalie mtoto, nikabeba mimba yake. Akanikana.

Huwezi amini kaka zangu, hapa nina mtoto mdogo, hata miaka miwili hajafikisha na nilianza kutoka na kuendelea kujiuza, mtoto akiwa na miezi mitatu tu. Mungu anamnusuru mwanangu, anaendelea vizuri.

Ijumaa: Kwahiyo kwa sasa unafikiri nini juu ya changamoto hizi za maisha yako? Bado unaendelea na shughuli hii?

Aziza: Uongo dhambi kaka, bado najiuza lakini nikipata mtaji wa biashara na matibabu nitaacha. Natakiwa kurudi tena MOI mwezi wa pili mwakani kwa ajili ya kuondolewa vyuma, nimeambiwa niende na laki tatu.

Kama umeguswa na kisa cha Aziza na unataka kumsaidia kwa hali na mali, wasiliana naye moja kwa moja kwa namba 0714 021105.

-GPL

No comments:

Post a Comment