Wednesday, 20 November 2013

Rage apinduliwa akiwa nje ya nchi

KLABU ya Simba imemuondoa madarakani mwenyekiti wake, Ismail Aden Rage.
Kamati ya Utendaji ya Simba iliyokutana jana, imefikia uamuzi wa kumsimamisha Rage akiwa nje ya nchi  na kumtangaza aliyekuwa Kaimu Makamu Mwenyekiti, Joseph Itang’are ‘Mzee Kinesi’ kushika nafasi hiyo ya juu zaidi katika klabu hiyo.
Akizungumza na Championi Jumatano, Mzee Kinesi alisema wamefikia maamuzi hayo kutokana na mwenyekiti huyo kwenda kinyume na makubaliano na Kamati ya Utendaji ya Simba.
Mzee Kinesi alisema maamuzi ya kumrejesha mwenyekiti huyo yatatolewa mara baada ya mkutano wa timu hiyo wa kupitisha mabadiliko ya katiba, utakaowashirikisha wanachama.
Makamu huyo aliitaja sababu ya kwanza ya kumuondoa mwenyekiti huyo kuwa ni; kuchukua maamuzi binafsi ya kuahirisha mkutano maalumu wa katiba uliotakiwa kufanyika Novemba, mwaka huu.
Pili; kuendesha klabu kwa kufanya maamuzi binafsi bila kuishirikisha kamati hiyo ya utendaji ambayo ilichaguliwa na wanachama.
Tatu; kuingia makubaliano ya mkataba na Azam TV kuonyesha vipindi vya Simba TV bila makubaliano ya kamati ya utendaji.
Nne; kumuuza kiungo wao mshambuliaji wa kimataifa, Emmanuel Okwi kwenye Klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia bila kulipwa hata senti.
Kamati ya utendaji ilimuagiza ahakikishe anarudi na fedha za malipo ya Okwi, lakini hakufanya hivyo na hadi sasa Simba inahaha kupata malipo hayo.
Mzee Kinesi alisema hayo ni baadhi ya mambo yaliyosababisha kumuondoa mwenyekiti huyo madarakani na nafasi ya makamu mwenyekiti ataikaimu mjumbe wa kamati ya utendaji, Swed Nkwabi.
“Kipengele namba 31(a) kilichopo kwenye katiba ya Simba kinasema kuwa kamati ya utendaji ina uwezo wa kuchukua maamuzi ya kumuondoa mwenyekiti madarakani pindi anapoenda kinyume na makubaliano ya kamati ya utendaji,” alisema Mzee Kinesi.
Juhudi za kumpata Rage azungumzie suala hilo zilikwama huku simu yake ikitoa majibu yanayoonyesha yupo nje ya nchi.
Baadaye ilielezwa yupo nchini Sudan na alikuwa njiani kwenda Marekani.

No comments:

Post a Comment