Saturday, 16 November 2013

Wazungu wawili wamshawishi Mholanzi Yanga


MAKOCHA wa kizungu, Muingereza Stewart Hall na Mfaransa Patrick Liewig wamemshauri Kocha Mkuu wa Yanga, Ernest Brandts kusoma alama za nyakati na kufuata nyayo zao. Aliyekuwa Kocha Mkuu wa Azam, Stewart Hall alisema,
“Nafikiri Kocha wa Yanga (Ernest Brandts) anajua kuwa mpira wa Tanzania ni mgumu, kila mtu anajiona anajua kazi ya ukocha. Inashangaza sana kuona kuwa unapokuwa kocha kwenye klabu, watu wanajifanya kujua kazi yako zaidi ya wewe unavyojua,” alisema.
“Kama Simba, Yanga na Azam watu wengi wanaingilia majukumu ya kocha, hivyo kunakuwa hakuna uhuru wa kazi na wakati mwingine wapenzi na viongozi wa soka hawawaheshimu makocha,” alisema Hall ambaye amesaini kuifundisha akademi mpya ya Sunderland ya Kidongo Chekundu na ile ya Elite Football Academy.
Naye Liewig aliyekuwa Simba, ameajiriwa kwenye akademi inayosimamiwa na Afrisoccer Consulting Limited ya Dar es Salaam akitokea Simba, atatua nchini Desemba Mosi kuanza kazi kwenye Orange Football Academy ya Zanzibar.
Liewig alisema: “Sasa ni wakati wa Brandts wa Yanga kuangalia wapi kutamfaa na nini anahitaji kwenye maisha yake, nafikiri akijipeleka kwenye soka la vijana atafurahi kwani klabu nyingi zinaendeshwa kisiasa bila ya kujali taaluma.”

Mwanaspoti

No comments:

Post a Comment