HII NDIO AJALI ILIYOUA WALIMU WAKUU WA 3 WA SHULE ZA MSINGI
WALIMU wakuu watatu waliotajwa kuwa ni Margaret Kimbo, Agrey
Kikwesha na Lanford Muhando kutoka shule mbalimbali za Tarafa ya Magole
wilayani Kilosa, wamefariki dunia baada ya gari walilokuwa wakisafiria
kupata ajali.
Mbali ya vifo vya walimu hao, ajali hiyo iliyotokea baada ya tairi
moja ya nyuma kupasuka, imesababisha majeruhi 17, baadhi yao wakiwa
katika hali mbaya.
Walioshuhudia waliliambia gazeti hili kuwa ajali hiyo mbaya ilitokea
juzi, majira ya saa 12 jioni katika Kijiji cha Mvumi na Rudewa, eneo la
Kisangata mkoani hapa.
Kwa mujibu wa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Magole, Koletha
Mhululu, walimu hao walikuwa wakisafiri kwenda wilayani Kilosa kuitika
wito wa ghafla wa mkuu wa wilaya hiyo kwa jambo la dharura ambalo
hawakulifahamu mapema.
Mwalimu Koletha alisema tairi la gari hilo lilipasuka na kusababisha
lipinduke mara nne na kusababisha baadhi yao kupoteza maisha hapo
hapo.
"Tulikuwa walimu na waratibu zaidi ya 17 tukielekea wilayani kuitika
wito wa mkuu wa wilaya, gari lilikuwa kasi na lilipopasuka tairi,
lilibilingika kama mara nne hivi,” alisema mwalimu huyo kwa uchungu na
kushindwa umalizia.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile, alisema
ajali hiyo ilitokea baada ya gari aina ya Toyota Hiace kupasuka tairi
la nyuma.
TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment