MABINGWA watetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Al-Ahly ya Misri
jana Jumapili walifanikiwa kulitetea taji hilo baada ya kuichapa Orlando
Pirates ya Afrika Kusini mabao 2-0 mechi iliyopigwa katika Uwanja wa
Arab Contractors, Cairo.
Mohammed Aboutrika aliipatia Ahly bao la kwanza
dakika ya 54 akiitumia vizuri pasi ya Abdullah Said ambaye mpira
alioupiga ulimbabatiza Gcaba kabla ya kumkuta mfungaji. Kuingia kwa bao
hilo kuliongeza ushindani kwa timu zote lakini ni juhudi za Ahly
zilizozaa bao dakika ya 78 mfungaji akiwa ni Ahmed Abdul Zaher
aliyeinasa pasi ya Ahmed Fathy.
Pirates ndio walioanza kwa kasi mechi hiyo, dakika
ya tatu tu walifanya shambulizi, Segolela alifumua shuti lakini mpira
huo uliokolewa kiulaini na kipa wa Ahly, Ekramy.
Katika mechi ya kwanza ambayo Ahly walikuwa ugenini matokeo yalikuwa sare ya bao 1-1.
Ahly ndiyo klabu yenye mafanikio katika michuano
hiyo mikubwa ya klabu Afrika, imebeba taji hilo mara nane wakati Pirates
imefanya hivyo mara moja tu, mwaka 1995.
No comments:
Post a Comment