KIGOGO mmoja mwenye ushawishi mkubwa Simba na anayewania
kugombea uongozi mwakani (jina tunalo), ameanza mazungumzo ya faragha na
wachezaji wawili wa Yanga.
Wachezaji hao ambao mikataba yao inamalizika ndani
ya miezi sita ijayo ni beki kisiki, Kelvin Yondani na winga mwenye
kasi, Simon Msuva.
Habari za ndani ambazo Mwanaspoti inazo ni kwamba
kiongozi huyo amepanga kuwasainisha wachezaji hao ambao kuanzia mwezi
ujao kikanuni watakuwa huru kufanya mazungumzo, kama sehemu ya kampeni
zake kwenye uchaguzi huo.
Yondani aliondoka Simba misimu miwili iliyopita na
kusababisha madhara kwenye safu ya ulinzi ya Wekundu hao wa Msimbazi
kwani wamekuwa wakikosa mbadala makini, ingawa kurejea kwa Joseph Owino
na usajili wa Gilbert Kaze vimewapa ahueni.
Mwanaspoti linajua kuwa Yondani na Msuva ingawa
wamegoma kukiri lakini wamekuwa wakishawishiwa na kigogo huyo wa Simba
na wameelekea kuridhia ndio maana hawajataka kupaparika kufanya
mazungumzo mapya na Yanga.
Msuva ambaye alijiunga na Yanga akitokea Moro
United iliyoshuka daraja amekuwa kwenye fomu kwa kipindi kirefu na jana
Jumatano alisema: “Nimebakiza muda wa miezi sita katika mkataba wangu na
Yanga, kisheria sina kipingamizi cha kufanya mazungumzo na timu yoyote
kuhusu hatma yangu ya soka, ila bado sijazungumza na Yanga kuhusiana na
suala la kuongeza mkataba mpaka sasa, nasubiri kumalizia mkataba wangu
na Yanga, endapo watafuata yale ninayoyataka, haitakuwa shida kuendelea
kuichezea Yanga, lakini kama itakuwa kinyume, itakuwa tofauti.”
Yondani kwa upande wake alisema mkataba wake
unamalizika mwakani mwezi Mei na suala la kuongeza mkataba litatokana na
makubaliano baina yake na timu yake ya sasa na hata timu nyingine
itakayomuhitaji.
“Mkataba wangu unamalizika baada ya msimu huu, kwa
sasa nipo huru kufanya maandalizi ya kazi yangu kwa kufanya mazungumzo
na timu zozote, ila kusaini Yanga nahitaji kupata muda wa kutafakari na
kama watafuata masharti yangu nitakubaliana nao,” alisema Yondani bila
kufafanua ni masharti yapi wala hakukiri kufuatwa na Simba.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Yanga, Abdallah
Bin Kleb ambaye mara kadhaa amekuwa akiigaragaza Simba katika vita ya
kuwania mchezaji, alisema kuwa hawajafanya mazungumzo na Yondani na
Msuva lakini hawana papara kwavile bado ni mali yao mpaka mwisho wa
msimu.
“Msuva na Yondani ni wachezaji wetu, bado wana
mkataba na sisi na si siri kwa kipindi ambacho wamebakiza tunajipanga
kujua tunafanya nini kwao, muda ukifika tutawajulisha, hatuna papara
katika usajili, tunachofanya sasa ni kusaka straika wa kigeni kutoka
nje,” alisema Bin Kleb kwa kujiamini huku akionyesha kutokuwa na presha
ya kuwapoteza wachezaji.
Habari za ndani zinadai kwamba baadhi ya wanachama
maarufu wa Simba wameanza mikakati ya chinichini kujipanga kuwania
uongozi wa juu klabu hiyo kwenye uchaguzi utakaofanyika baada ya
kumalizika kwa ligi mwakani.
Mwaspoti
Mwaspoti
No comments:
Post a Comment