Amiri Jeshi Mkuu, Rais Jakaya Kikwete amewapandisha vyeo maofisa
77 wa Jeshi la Polisi kutoka Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) kuwa
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP).
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na
Msemaji wa jeshi hilo, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), Advera Senso
imesema waliopandishwa vyeo ni pamoja na makamanda wa polisi wa mikoa
mbalimbali nchini.
Aliwataja baadhi ya maofisa hao kuwa ni Mkuu wa
Upelelezi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Ahmed Msangi, Kamanda wa
Polisi wa Mkoa wa Temeke, Engelbert Kiondo na Kamanda wa Polisi Mkoa
wa Ilala, Marietha Minangi.
Makamanda wengine waliopandishwa vyeo na mikoa yao
kwenye mabano ni Diwani Athumani (Mbeya), Frasser Kashai (Kigoma),
Geofrey Kamwela (Singida), Faustine Shilogile (Morogoro), David Misime
(Dodoma) na Ferdinand Mtui (Mara).
Wengine ni Costantine Massawe (Tanga), Leonard
Paul (Geita), Ulrich Matei (Pwani), Evarist Mangala (Shinyanga)
Deusedit Nsimeke (Ruvuma), Fulgence Ngonjani (Njombe), George Mwakajinga
(Lindi) na Dhahiri Kidavashari (Katavi).
Wengine ni baadhi ya makamanda wa vikosi, wakuu wa
vitengo, Mkuu wa Chuo cha Taaluma ya Polisi Moshi na Mkuu wa Chuo cha
Taaluma ya Polisi Dar es Salaam.
Mara ya mwisho kwa maofisa wa jeshi hilo
kupandishwa vyeo ilikuwa Mei mwaka kuu wakati makamishna wawili na
manaibu kamishna 19 walipoteuliwa.
Miongoni mwa walioteuliwa walikuwa Kamanda wa
Polisi Kanda Maalumu ya Dar e Salaam, Suleiman Kova na Kaimu Mkurugenzi
wa Idara ya Upelelezi, Isaya Mngulu walipopandishwa cheo kutoka Naibu
Kamishna (DCP) na kuwa Kamishna wa Polisi (CP).
Miongoni mwa waliopandishwa vyeo na kuwa manaibu
kamishna wa Polisi ni Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed
Mpinga, Thobias Andengenye na Michael Kamuhanda.
No comments:
Post a Comment