Siku chache baada ya kumalizika kwa Mkutano wa 13 wa Bunge,
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Deo
Filikunjombe amesema kamati yake inashindwa kutekeleza majukumu yake
ipasavyo kutokana na kubanwa na Ofisi ya Spika.
Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya Mbunge wa
Nzega (CCM), Dk Hamisi Kigangwala kuongoza harakati za kumng’oa Spika wa
Bunge Anne Makinda kwa madai kuwa anaongoza Bunge kwa upendeleo na hasa
kwenye uendeshaji wa kamati. Alikusanya saini za wabunge wapatao 30 ili
waunge mkono hoja yake, ambayo kwa sasa inashughulikiwa na Kamati ya
Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge.
Filikunjombe ambaye pia ni Mbunge wa Ludewa (CCM),
alisema hayo jana wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya kuwajengea uwezo
Wajumbe wa PAC na Kamati ya Bunge ya Serikali za Mitaa (LAAC),
yaliyohudhuriwa pia na Ndugai pamoja na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh.
Alisema mara nyingi kamati hiyo inapozihoji idara
mbalimbali, Spika Makinda au Naibu wake, Job Ndugai wamekuwa wakiwapigia
simu na kuwataka kutoruhusu vyombo vya habari kusikiliza majadiliano
hayo, kitendo alichosema kuwa kinazorotesha uwajibikaji.
“Mara nyingi tumekuwa tukipokea simu kutoka kwao
zinazolalamikia utendaji wa kamati hii,” alisema na kuongeza: “Hatua
hiyo inatokana na kamati (PAC) kuwa na tabia ya kuruhusu vyombo vya
habari kuingia katika vikao vyetu wakati tunapokuwa tunahoji watendaji
wa idara mbalimbali. Wamekuwa wakitupigia simu na kututaka tusifanye
hivyo.”
Ndugai alisema kanuni za Bunge zinaruhusu vyombo
vya habari kushiriki katika vikao vya kamati za Bunge lakini wanaandaa
utaratibu wa ushiriki wao.
“Kuanzia sasa tunajaribu kuangalia namna ya kuweka
utaratibu ili kuvisaidia vyombo vya habari kupata taarifa za matumizi
ya fedha za umma bila ya kuathiri utendaji wa kamati,” alisema.
Filikunjombe alipendekeza kubadilishwa kwa kanuni
ili vikao vya PAC na LAAC virushwe moja kwa moja katika televisheni kama
ilivyo mikutano ya Bunge ili kama kuna mtu anasema uongo wananchi
wamwone.
Alisema hali hiyo itasaidia watendaji kuongeza
uwajibikaji na uwazi katika matumizi ya fedha za umma… “Inashangaza…
maana tukiwaita watendaji kujieleza mbele ya kamati juu ya matumizi ya
fedha tunapigiwa simu na Spika Makinda au Naibu wake, hii inaondoa dhana
nzima ya uwajibikaji,” alisema.
Alisisitiza kuwa idara hizo huwa zinaomba fedha za
umma bila kificho kwa nia ya kuzitumia kwa mambo ya msingi lakini
ameshangazwa na hofu ya viongozi kuhojiwa wakati vyombo vya habari
vikiwapo.
Alisema umefika wakati kwa Ofisi ya Spika kuziamini kamati na kuziacha zifanye kazi zake kwa umakini ili kuwa na uwajibikaji.
“Ni vizuri kamati hizi mbili zikaachwa zifanye
kazi zake kwa sababu zina umuhimu mkubwa katika usimamizi wa fedha za
umma,” alisema Filikunjombe.
Mwananchi
Mwananchi
No comments:
Post a Comment