Wednesday, 13 November 2013


Upinzani umegundua kwamba Serikali ya Jubilee imeanza kuonyesha kucha zake miezi michache baada ya kujifanya kwamba inafuata sheria na kulinda Katiba. Ilifanya hivyo kwa kuteua Baraza la Mawaziri inavyotakiwa kisheria, lakini sasa mambo yamebadilika.
Uhuru na Makamu wake,William Ruto, wameonyesha kuwa hawajali lolote zuri linaloiweka Kenya kwenye jukwaa la mataifa yanayowalinda wananchi wake. Kwa wiki moja iliyopita, Upande wa Serikali bungeni umepitisha miswada miwili inayorudisha nyuma hatua nzuri zilizokuwa zimepigwa.
Kumekuwa na kilio kikuu kutoka kwa Wakenya kuhusu hatua ya Serikali kutaka kuzima uhuru wa wanahabari na pia kukata msaada kwa mashirika yasiyo ya kiserikali kutoka kwa mashirika ya maendeleo ya nchi za Ulaya na Magharibi.
 Si jukumu la upinzani kuisifu Serikali na kuchochea maendeleo. Huu si wakati wa kupakana mafuta kwenye mgongo wa chupa kwani mshuka ngazi na mpanda ngazi kamwe hawawezi kushikana mikono.
  Jukumu lake ni kuhakikisha Serikali inafuata mkondo unaofaa inapoendesha shughuli zake. Ni jukumu la kusukuma Serikali ili izingatie ahadi zake zote ilizotoa kwa Wakenya wakati wa kampeni na uchaguzi na hatimaye wakati wa kuapishwa kwake Uhuru na Ruto Aprili 9, 2013.
Kuna orodha ndefu ya mambo yasiyofurahisha wengi nchini, na chimbuko la haya yote ni Serikali ya Jubilee. Wakenya bado wanajiuliza maswali kuhusu jinsi mkuu wa majeshi alivyokuwa amekana kwamba kikosi chake hakikupora mali wakati wa mashambulizi ya Westgate.
Maji yalipozidi unga, Serikali ilikiri kwamba kweli, wanajeshi walikuwa wamepora. Kwanini Wakenya wachukuliwe kana kwamba ni majuha? Mbona Serikali haikukiri mara moja kwamba makosa yalifanyika badala ya kujaribu kuficha ukweli?
Muswada wa ushuru wa chakula na bidhaa nyingine muhimu ulipelekea kupanda kwa gharama ilhali mapato ya wananchi ni yale yale. Baada ya kilio kutoka kwa raia, Serikali ilitoa sababu kwamba haikuwa inalenga bidhaa muhimu kama vile maziwa na mikate walipoupitisha muswada huu.
Sote twafahamu ni kina nani wanaoshikilia sekta ya maziwa na wangefaidi kutokana na kuongezeka kwa bei ya maziwa na bidhaa nyingine.
Isitoshe, kuna maswali mengi kuhusu jinsi pesa za umma zinavyotumiwa. Tangu vikao vya kesi zinazomkabili Ruto ianze The Hague zaidi ya mwezi mmoja uliopita, wabunge na wafanyakazi wa umma wamekuwa wakimtembelea kiongozi huyu kila wiki ili kumpa moyo kortini.
Je, wabunge na wafanya kazi wa umma wanaosafiri kila mara kumtembelea Makamu wa Rais wanafanya hivyo kwa kujigharamia au fedha za umma ndizo zinatumiwa?
Pia, Waziri wa Masuala ya Nchi za Nje, Amina Mohammed amekuwa kiguu na njia tangu ateuliwe. Kazi ya kutumikia wananchi imewekwa kando badala yake kesi ya Uhuru imepewa kipaumbele.
Mohammed ametembelea nchi nyingi kutafuta uungwaji mkono kwa kesi hizi. Uhuru na Ruto walikuwa wamewahakikishia wananchi wakati wa kampeni na hata walipokuwa wakifanya kampeni kwamba, kesi zao ni za kibinafsi. Lakini sasa zimekuwa za kitaifa na hata kimataifa. Wakenya wangetaka kujua pesa hizo zote za nauli na kadhalika zinalipiwa na nani.
Shirika moja lisilo la kiserikali, Mars Group linaunga mkono juhudi za Upinzani za kutaka kujua jinsi safari hizi za kila mara zinavyogharamiwa. Mkurugenzi Mkuu wa Mars Group Kenya,  Mwalimu Mati anataka Uhuru aeleze ikiwa matumizi ya pesa kwenye shughuli za kibinafsi kama hizi zilijadiliwa kama muswada katika Bunge la kitaifa na kupitishwa.
Upinzani ungetaka kujua mfuko wa fedha unaotumiwa na Uhuru na Ruto kuzuru nchi mbalimbali za Afrika kukutana na viongozi wa kisiasa barani ili wawaunge mkono kuhusiana na kesi za Hague.
Rais mwenyewe alizuru Botswana Jumatano wiki jana na kukutana na Rais Ian Khama kujadili kile maofisa wao wametaja kama masuala ya uhusiano ya nchi hizi mbili, barani na kimataifa.
Itakumbukwa hata hivyo kwamba, Botswana inapinga vikali jaribio la Rais Uhuru kutaka kesi dhidi yake kuahirishwa ama kufutiliwa mbali. Zaidi ya hayo, Botswana ilikuwa imetishia kumnasa Uhuru na kumkabidhi mikononi mwa Mahakama ya Kitaifa ya Uhalifu (ICC) ikiwa atatembelea nchi hiyo.
Ilibidi Uhuru amtembelee Khama kumshawishi amuunge mkono ili kesi yake iahirishwe. Haijulikani kama kiongozi huyo alikubali ama la.
Wiki jana Rais aliwatuma mawaziri Mohammed, Najib Balala na Fred Matiang’I kutafuta uungwaji mkono katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusiana na kesi zinazomkabili Uhuru.
Uhuru pia amewapigia simu si haba Rais Barack Obama wa Amerika na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon.
Matokeo ya juhudi hizo yamebakia kuwa siri kubwa ya Ikulu
Hata hivyo, viongozi wa upinzani sasa wanamtaka Uhuru aubebe msalaba wake mwenyewe kwa kuhudhuria vikao vya ICC kuanzia Februari 5, mwaka ujao.
Viongozi hao hawataki kumpaka Uhuru mafuta kwa mgongo wa chupa jinsi wanasiasa wa chama chake cha Jubilee wanavyofanya. 
Upinzani umesimama kidete na kuiambia ICC isisite kumtupa kizimbani Uhuru ajibu kesi zinazomkabili. Ameambiwa wazi afikirie vizuri athari za yeye kususia kesi hizo. Je, Kenya itaendelea namna gani ikiwa yeye atakosa kufika kizimbani?
Mohamed Dida ambaye pia aligombea naye urais, hakutaka kuachwa nyuma. Anasema Uhuru na Ruto wana shida nyingi sana na hata hawana wakati wa kuwatumikia Wakenya. Anasema, tulionywa na Amerika kabla ya uchaguzi kwamba tukichagua Uhuru na Ruto tungejuta na sasa tumejuta.
Dida anashangaa kwamba licha ya onyo hilo Wakenya 6,000,000 walimchagua Uhuru. Kweli sikio la kufa halisikii dawa.
Dida anasema Uhuru amefanya vibaya katika kuendeleza nchi na yaweza kupata alama nne kwa kumi.Mwezi jana Martha Karua ambaye pia alipigania urais alisema kwamba hajuti kamwe kwa kusaidia ICC kupata ushahidi dhidi ya viongozi hao wawili kuhusu jinsi walivyochangia katika mapigano ya 2007/2008.

Mwananchi

No comments:

Post a Comment