MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jana Jumatatu ilimwachia huru
Mwenyekiti wa Chama cha Soka Pwani (Corefa), Hassan Othman ‘Hassanol’
(45).
Hata hivyo Hassanol anaendelea kusota mahabusu akikabiliwa na kesi nyingine ya kukutwa na pembe za ndovu.
Pamoja na Hassanol wengine walioachiwa na mahakama
hiyo ni mfanyabiashara wa madini, Najim Msenga na Wambura Mahega baada
ya kuwaona hawana hatia katika mashitaka matatu yaliyokuwa yakiwakabili
likiwamo la wizi wa shaba yenye thamani ya Sh 333 milioni.
Najim ambaye ni mfanyabiashara wa madini na Mjumbe
wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, aliishukuru mahakama kwa kutenda
haki, kuangalia ukweli huku akidai kwamba tangu azaliwe hajawahi kuiba.
Akisoma hukumu hiyo, ambayo imeandaliwa na Hakimu
Devotha Kisoka na kusomwa na Hakimu Sundi Fimbo, washitakiwa walikuwa
wakikabiliwa na mashitaka matatu ya kula njama, kuiba na kupokea mali ya
wizi.
Mali hizo ni tani 26.475 za madini aina ya shaba
zenye thamani ya Sh333 milioni zilizokuwa zikisafirishwa kutoka Zambia
kwenda Dar es Salaam, mali ya Kampuni ya Liberty Express Tanzania
Limited.
Hakimu Fimbo alisema ushahidi wa upande wa
mashitaka haujathibitisha kama walikula njama kwa sababu hakuna mahali
katika ushahidi huo unaoonyesha kuwa washitakiwa waliwahi kuwasiliana au
kupanga njama ya kutenda kosa kwa njia yoyote ile.
Alisema dereva wa lori lililobeba shaba iliyoibwa
angeweza kuwa shahidi lakini upande wa mashitaka haukumwita kueleza wapi
shaba hiyo ilipelekwa kwa sababu ilitakiwa kupelekwa Kurasini lakini
ikapelekwa kwenye yadi Bahari Beach.
Hakimu huyo pia alisema hakuna upelelezi uliowaonyesha washitakiwa hao wakiiba au wakipokea hizo shaba.
Kwa upande wa Najim wakati wa tukio hakuwepo, Dar
es Salaam alikuwa Tanga kwenye msiba na upande wa mashitaka haukuwa na
shida na hilo na kwamba yadi ni yake na yadi hiyo ina meneja ambaye
ameajiriwa lakini upande wa mashitaka haukumwita kuwa shahidi.
“Kutokana na ushahidi huo pamoja na utetezi wa washitakiwa, mahakama inawaona hawana hatia wapo huru,’’ alisema hakimu.
Mwanaspoti
Mwanaspoti
No comments:
Post a Comment