WATAALAMU wa hesabu wana usemi wao wanaoupenda ‘Namba
haziongopi’. Ukirudisha usemi huo kwenye tathimini ya mzunguko wa kwanza
wa Ligi Kuu Tanzania Bara, lugha nyepesi unayoweza kusema ni kwamba
‘hakuna kama Yanga’.
Sahau kwamba imemaliza ikiwa kileleni na pointi
zake 27. Takwimu za Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL), zimethibitisha
kwamba Yanga imeongoza takwimu zote kuanzia mapato mpaka idadi ya
mashabiki walioingia uwanjani.
Takwimu zilitolewa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa TPL,
Silas Mwakibinga, ni kuwa Yanga imekusanya kiasi cha Sh334.2 milioni
katika mechi 13 za mzunguko huo. Katika takwimu hizo, Simba SC ni ya
pili kwa kupata Sh304 milioni huku timu iliyopanda daraja msimu huu,
Mbeya City, ikiipiku Azam FC kwa kushika nafasi ya tatu kwa kujikusanyia
Sh83.8 milioni. Azam imekusanya Sh67.1 milioni.
Nyingine na fedha zilizokusanya katika mabano ni
Coastal Union (Sh65. 7 milioni), Mtibwa Sugar (Sh49.9 milioni), Ruvu
Shooting (Sh46.1 milioni), Tanzania Prisons (Sh38.1milioni), JKT Ruvu
(Sh36.1 milioni), Ashanti United (Sh35.7 milioni), Rhino Rangers
(Sh31.1milioni), Mgambo JKT (Sh25.8 milioni), Oljoro JKT (Sh20.8
milioni) na Kagera Sugar (Sh18.5 milioni).
“Huu ni mwanzo tu wa kusimamia ligi na mpaka sasa
hatujafikia lengo letu, tunataka kuona kila timu inakuwa na uwiano sawa
wa makusanyo na kama kuzidiana, basi iwe kiasi kidogo, tumefurahishwa na
mwenendo wa Mbeya City ambao wamefanya mambo makubwa japo wapo katika
msimu wa kwanza,” alisema Mwakibinga.
Kwa upande wa mashabiki walioingia viwanjani,
Yanga pia imekuwa kinara kwa kuingiza mashabiki wengi katika mechi.
Jumla ya mashabiki 107,890 wa timu hiyo wameingia katika mechi na
kufuatiwa na Simba ambao wameingiza mashabiki 97,364 mpaka mwisho wa
mzunguko huo.
Timu ya Mbeya City imezidi kung’ang’ania nafasi ya
tatu na kuendelea kuitambia Azam FC kwa kuingiza mashabiki 43,439
tofauti na Azam ambao mpaka sasa wameingiza mashabiki 30,236.
Nyingine ni Coastal Union (mashabiki 27,880),
Mtibwa Sugar (20,794), Rhino Rangers (20,263), Prisons (19,923), Ruvu
Shooting (19,000), JKT Ruvu (16,095), Ashanti United (16,093), Mgambo
(11,726) na JKT Oljoro (10,430).
Kwa mujibu wa Mwakibinga, jumla ya Sh 2.4 bilioni
zimekusanywa katika mzunguko huo wa kwanza. Kiasi hicho ni ongezeko la
Sh599. 5 milioni katika mzunguko wa kwanza wa msimu uliopita.
“Hii ni historia na hasa ukizingatia kuwa baadhi
ya mechi zimekuwa zikionyeshwa ‘laivu’ katika televisheni na baadhi ya
mashabiki kuangalia kupitia luninga zao, lakini bado tumezidi kupata
makusanyo makubwa,” aliongeza Mwakibinga.
“Haya ni matokeo mazuri ya kuzinadi mechi za ligi
na mfano mzuri mechi ya Yanga na Mbeya City ambayo iliweka historia kwa
kuingiza Sh100 milioni na huku tiketi zikiwa zimemalizika kufikia saa
5:00 asubuhi ya siku ya mchezo.”
Kwa upande wa viwanja, Uwanja wa Taifa unaongoza
kwa kukusanya fedha nyingi mpaka sasa ambapo kiasi cha Sh1.8 bilioni
kimepatikana hapo, kiwango hicho ni sawa na asilimia 75 ya mapato yote
ya mzunguko wa kwanza.
Mwanaspoti
Mwanaspoti
No comments:
Post a Comment