Marekani imetoa ripoti inayozungumzia usafirishaji wa binadamu
ya mwaka 2013, huku ikiitaja Tanzania kuwa kinara wa kunyanyasa
wasichana, kuwatumikisha katika ngono na usafirishaji wa binadamu.
Ripoti hiyo iliyotolewa na idara ya nchi hiyo
inayohusika na diplomasia (US Department of State, Diplomacy in Action),
pia inaitaja Tanzania kuwa ni kitovu cha njia ya kusafirisha wanawake,
watoto na wanaume ambao hutumikishwa kwenye kazi za mashambani na
biashara ya ngono.
Ripoti hiyo iliyozinduliwa Julai mwaka huu na
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Seneta John Kerry inaweka bayana
kwamba biashara ya usafirishaji wa binadamu hufanywa na baadhi ya ndugu
na marafiki ambao hutoa ahadi kwa wahusika kwamba wanakwenda kuwasomesha
au kuwatafutia ajira nzuri mijini.
“Unyonyaji wa wasichana wadogo na utumikishaji
majumbani ndilo tatizo linaloongoza, ingawa kesi za watoto kusafirishwa
kwa ajili ya biashara ya ngono katika mpaka wa Tanzania na Kenya
zinaongezeka. Pia, wasichana wananyonywa kwenye maeneo ya utalii,”
inasema sehemu ya ripoti hiyo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, watoto kutoka Burundi
na Kenya, watu wazima kutoka Bangladesh, Nepal, Yemen na India
wanatumikishwa kufanya kazi kwenye sekta za kilimo, madini na majumbani
nchini Tanzania.
“Baadhi ya raia kutoka nchi jirani huingia
Tanzania kwa hiari yao, lakini hulazimishwa kufanya kazi majumbani kabla
ya kupelekwa kutumikishwa kwenye biashara ya ngono Afrika Kusini, Ulaya
na Mashariki ya Kati,” inaeleza.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Angela Kairuki
alimtaka mwandishi kumtumia ripoti hiyo kwa njia ya baruapepe ili aweze
kuisoma na kuitolea maelezo.
Alipotafutwa siku ya pili, alisema kuwa ameipokea
na kuikabidhi ofisi ya Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka (DPP) ili ifanyiwe
kazi na baadaye kutoa majibu.
“Ripoti niliipata nikaikabidhi ofisi ya DPP kwa
kuwa wao ndio wanaoweza kuitolea maelezo baada ya kuisoma. Maoni yangu
lazima yawe ya kitaalamu siwezi kusema bila kupata taarifa kutoka kwao,”
alisema.
Mwananchi
Mwananchi
No comments:
Post a Comment