KATIKA hali ya kutatanisha, straika wa Yanga, Hamis Kiiza raia
wa Uganda amekuja juu na kususia uamuzi wa kutolewa nje na benchi la
ufundi linaloongozwa na Mholanzi Ernest Brandts.
Kiiza alitolewa katika mechi yao na JKT Oljoro Alhamisi iliyopita ambayo walishinda kwa mabao 3-0.
Lakini pamoja na kitendo hicho, Kocha Msaidizi wa
Yanga, Fred Minziro amemtetea na kusema ni hali ya kawaida kwa mchezaji
kuchukia anapotolewa nje.
Kiiza ana mabao manane akimfukuzia kwa karibu
Amissi Tambwe wa Simba anayeongoza kwa mabao kumi. Kiiza alichukia baada
ya kutolewa kwenye mchezo huo mara baada ya kipindi cha kwanza
kumalizika na nafasi yake aliingizwa, Jerry Tegete aliyecheza dakika 45
za kipindi cha pili jambo ambalo hakulifurahia na ndipo akaamua kutoa la
moyoni.
Katika kuonyesha hasira, alitoka chumba
wanachopumzikia wachezaji wote uwanjani na kwenda nje kwenye korido na
kukaa akiwaacha wenzake vyumbani huko wakizungumza pamoja na bechi la
ufundi na uongozi wa timu akiwemo Mwenyekiti wao, Yusuph Manji
aliyeingia kuwapongeza.
Akiwa ameketi nje, Kiiza alikuwa akilalamika kwa
kutoa maneno makali akiashiria kuchukizwa kwake: “Nimekuwa nacheza
pembeni kama winga wa kushoto lakini kwa juhudi zangu nafunga, nimecheza
katikati leo (Alhamisi) kidogo tu kwa sababu sijafunga nalaumiwa na
kutolewa nje.”
“Mimi sijapenda na sijui tatizo ni nini. Kabla ya
mechi niliwaambia kama watanitoa leo wasinichezeshe na kama
wananichezesha wasinitoe,” alisema Kiiza.
Baadaye akaongeza maneno haya bila kumtaja ni nani
anayemzungumzia kabla ya kuondoka kwa hasira: “Nitaongea na mabosi
wake, ama zangu ama zake.”
Minziro kwa upande wake alisema: “Kitendo cha
Kiiza kuchukia kutolewa ni jambo la kawaida kwa mchezaji, hakuna
anayependa kutolewa kwenye mechi.”
Baadhi ya wachezaji wamesema, Kiiza alichukizwa na
kitendo cha kutolewa nje kwani alitaka kubaki ili afunge mabao
amkaribie Tambwe na kumaliza vizuri mzunguko wa kwanza.
Chanzo Mwanaspoti
Chanzo Mwanaspoti
No comments:
Post a Comment