Ofisa Uhamiaji wa Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Kilimanjaro
(Kia), mwenye cheo cha Sajenti ameingia matatani baada ya kutuhumiwa
kumtukana matusi ya nguoni Rais Jakaya Kikwete.
Kutokana na kashfa hiyo, Polisi mkoani
Kilimanjaro, wamependekeza ofisa huyo achukuliwe hatua za kinidhamu kwa
kukiuka kiapo cha utii kwa Rais wakati akihitimu mafunzo yake.
Tukio hilo ambalo limefanywa siri kubwa, lilitokea
Oktoba Mosi mwaka huu 10:00 alasiri katika Baa ya G5 iliyopo
Bomang’ombe wilayani Hai na jalada la uchunguzi namba BNG/IR/3498/2013
limeshafunguliwa.
Mkuu wa Uhamiaji wa Mkoa wa Kilimanjaro, Johannes Msumule, alikiri kuwapo kwa tukio hilo na kwamba wanalifanyia kazi.
Msumule alisema ofisi yake inafahamu tukio hilo
lakini akataka lisiandikwe magazetini kwanza kwa maelezo kuwa
watalitolea taarifa baadaye.
Alisema juzi alikuwa jijini Dar kushughulikia suala hilo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz hakupatikana jana kuzungumzia tukio hilo.
Habari kutoka polisi zilisema ofisa huyo alitoa matusi ambayo hayaandikiki dhidi ya Rais.
Inasemekana alifanya hivyo baada ya kutakiwa kulipa ankara ya vinywaji alivyokuwa amehudumiwa katika baa hiyo.
“Alimtolea matusi mhudumu aliyempelekea bili na baadaye Rais kwa kumtolea matusi ya nguoni,” kilisema chanzo chetu cha habari.
Inasemekana baada ya kutoa matusi hayo, wananchi
waliokuwa katika eneo hilo walichukizwa na kupiga simu polisi na kwa
mkuu wa upelelezi wa wilaya hiyo.
Mwananchi
Mwananchi
No comments:
Post a Comment