SAA chache kabla ya kusaini mkataba wa kuichezea Yanga, Juma
Kaseja alimpigia simu kipa wa Yanga, Ali Mustapha ‘Barthez’ na kumueleza
kuhusu mchongo mzima wa klabu hiyo ya Jangwani kumuhitaji.
Barthez baada ya kupokea simu hiyo na kusikiliza alichoambiwa na Kaseja akamjibu; “Njoo tufanye kazi ndugu yangu.”
Kwa mujibu wa Barthez, hata kabla ya dili hilo,
mara kwa mara huwa anawasiliana na Kaseja kuelezana mambo mbalimbali ya
kimaisha hivyo hakuona ajabu kupokea simu ya kipa mwenzake.
“Unajua Kaseja huwa tunawasiliana mara kwa mara na
hata alipotaka kusaini Yanga alinipigia kunielezea jambo hilo na mimi
nikamjibu aje tufanye kazi pamoja hakuna tatizo,” alisema Barthez.
Barthez alisema kimsingi haoni tatizo kwa Kaseja
kujiunga na Yanga kwani anaamini kila mmoja anaweza kucheza kwa nafasi
yake huku mazoezi yakiwa ni silaha kubwa kwao.
“Tupo watatu hapa, kila mmoja anataka kucheza
hivyo ni jukumu letu kujituma katika mazoezi na atakayeonekana kuwa bora
ndiye atakayecheza hivyo sina shaka juu ya nafasi yangu,” alisema
Barthez, ambaye yumo katika kikosi cha Taifa Stars.
Ujio huo wa Kaseja unaifanya Yanga kuwa na makipa
watatu sasa katika kikosi chake wengine wakiwa ni Barthez na Deogratius
Munishi ‘Dida’ ambao wote kwa pamoja wamewahi kuwa makipa wa Simba.
Kaseja amesajiliwa kwa dau la Sh 40 milioni na mkataba wake utadumu kwa miaka miwili.
No comments:
Post a Comment