Tuesday, 12 November 2013

BARUA NZITO: WASANII TUAMKE, TUNANYONYWA NGUVU ZETU!

Najua maswali yamekuwa mengi kwa kuwa kuna watayarishaji wengi wa filamu nchini wanaohangaika usiku na mchana ili kupata mkataba wa kufanya kazi chini ya kampuni hiyo kwa kuwa Steps Entertainment ndiyo kampuni ya usambazaji inayolipa vizuri zaidi kuliko makampuni mengine yote kwa sasa.
Leo nimeamua kuongea walau kidogo. Kwanza nikiri kuwa maneno ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dk. Jakaya Kikwete aliyotamka siku alipoiita Ikulu kamati ya mazishi ya marehemu Steven Kanumba ndiyo yamekuwa yakinisukuma sana hadi kufikia uamuzi huu mzito.
Kati ya waliounda kamati hiyo iliyoitwa Ikulu, mimi nilikuwa katibu, mwenyekiti alikuwa Gabriel Mtitu ‘Mtitu Game’, pia kulikuwa na wajumbe wengine kama Ruge Mutahaba, Asha Baraka, Jacob Steven ‘JB’ na Mzee Chilo. Baada ya kuongea mengi kuhusiana na msiba wa Kanumba na mazishi yake, Rais aliuliza: “Hivi marehemu Kanumba kaacha filamu ngapi?”
Kwa aibu tulimjibu, hajaacha hata filamu moja, zote ni za msambazaji wake na hata mbili ambazo zilikuwa hazijatoka yaani Ndoa yangu na Love & Power tayari zilikuwa ni za msambazaji kutokana na aina ya mkataba tunayoingia na msambazaji.
Mhe. Rais alisikitika sana, akatuambia kuwa yeye hawezi kutumia nguvu kutukataza kuuza mali zetu lakini angependa kuona kuwa tunamiliki wenyewe filamu zetu na tutakapoona tumekwama tumwambie. Alisema, kuuza haki zetu ni kama kuuza utu wetu. Maneno yake yalinichoma sana.
Mimi ni msanii wa kwanza kufanya kazi na kampuni hiyo kama mtayarishaji wa filamu. Sinema yao ya kwanza kuisambaza ilikuwa ni Jeraha la Ndoa ambayo niliitengeneza mimi. Na kwa kuthibitisha hilo, mwaka huu kampuni hiyo ilitoa tuzo ya heshima kwa kampuni yangu ya 5 Effects Movies Ltd kwa ajili hiyo.
Nasikitika kukiri kuwa filamu zote nilizozitengeneza kisha zikasambazwa na Steps, siyo zangu tena. Kampuni hiyo imekuwa ikinunua haki zote za filamu wanazopelekewa kwa ajili ya kuzisambaza kwa hiyo baada tu ya kusaini mkataba wao unakuwa huwezi kufaidika tena na chochote kutokana na mauzo au faida nyingine zinazotokana na filamu yako.
Kwa aina ya mikataba ambayo wasanii na watayarishaji tunaingia na Steps, sisi tumekuwa ni wasimamizi tu wa filamu zao, yaani ni kama manyapara kwenye mashamba ya mkonge wakati wa ukoloni. Ni waajiriwa tusio na mafao ya uzeeni.
Kwa taarifa tu ni kwamba filamu zote mnazoziona mitaani zikisambazwa na kampuni siyo za hayo makampuni yanayotajwa kutengeneza filamu hizo bali ni filamu za Steps. Ndiyo maana hata ukienda kwenye Chama cha Hakimiliki Tanzania (COSOTA) utakuta wasanii wakubwa hawamiliki kabisa filamu lakini Steps inamiliki filamu zaidi ya 400.
Kifupi ni kuwa hadithi ni zetu, sehemu za kuigizia ni zetu, tunaigiza sisi, tunarekodi na kuhariri sisi lakini filamu ni za Steps Entertainment na ndiyo maana hata kampuni ya marehemu Steven Kanumba ‘Kanumba The Great Film’ imesambaratika baada ya kifo chake na mama yake akikabiliana na ugumu wa maisha lakini filamu za Kanumba bado zinatesa kwenye soko la filamu ndani na nje ya nchi.
Nawashangaa watu wanaomshutumu mama mzazi wa Kanumba kuwa amemaliza mali za mwanaye na sasa anaishi kwa kufadhiliwa na Lulu (Elizabeth Michael), wangejua kilicho nyuma ya pazia wangemuonea huruma badala ya kumshutumu.
Wakati Steps wanakiri kuwa filamu iliyowahi kuuza sana katika historia ya kampuni yao ni Ndoa Yangu ya Kanumba, hawasemi kuwa familia yake imenufaika vipi zaidi ya kupewa tuzo.
Wiki ijayo nitakuwa hapa kumalizia waraka wangu.
Willium Mtitu.

Chanzo Risasi

No comments:

Post a Comment