Monday 27 January 2014

Eto’o alivyokutana na mtoto kipenzi chake


SAMUEL Eto’o anakumbuka mara ya kwanza alipomwona shujaa wake wa kwenye soka. Kipindi hicho, Eto’o alikuwa na umri wa miaka minane tu, akawa anakwenda uwanjani Douala kumshangaa Roger Milla kwenye mazoezi ya timu ya taifa ya Cameroon.
Hiyo ilikuwa miezi michache tu kabla ya Milla kwenda kwenye fainali za Kombe la Dunia mwaka 1990 zilizofanyika Italia.
Uwanjani hapo kwenye mazoezi, Eto’o alishinda kutwaa nzima, kuanzia saa 2 asubuhi hadi saa 10 jioni ili tu amwone Milla. Straika huyo mkongwe, alichokuwa akifanya ni kutabasamu tu kila alipomtazama Eto’o.
Milla alikuwa akionyesha ujuzi wake ndani ya uwanja, akawa anapandisha soksi zake kabla ya nyingine kwenda kuzitundika kwenye uzio karibu na ulipokuwa mkono wa baba yake Eto’o. Akiwa mtoto, Eto’o alibaki kushangazaa tu, huku Milla alimpungia mkono kila mara.
“Nilisubiri kwa muda mrefu sana kumtazama na nilipomwona ilikuwa furaha kubwa sana kwangu. Alikuwa shujaa wangu,” anasema Eto’o akimzungumzia Roger Milla, mwanasoka mashuhuria Cameroon na Afrika kwa ujumla.
Wakati Eto’o akikumbuka hilo lililowahi kumtokea utotoni na jinsi alivyopambana kutimiza ndoto zake kuwa kweli, wiki iliyopita hadithi ilibadilika na yeye kukawa na mtoto anayemhusudu na kuwa shujaa wake.
Alipokuwa mazoezini, Eto’o alipata ugeni wakati alipotembelewa na mtoto, Nathan Thomas, ambaye straika Eto’o ndiye shujaa wake.
Mtoto Nathan ana umri wa miaka 10 na anasumbuliwa na ugonjwa wa ini, lakini mara zote amekuwa akimfuatilia Eto’o kwenye klabu zote anazocheza tangu akiwa Inter Milan, Anzhi na sasa Chelsea.
Nathan si shabiki wa Chelsea, bali ni shabiki wa Eto’o na hilo limetokea baada ya kumwona kwenye michezo ya kompyuta wakati huo alipokuwa akiichezea Barcelona ya Hispania.
Tangu hapo mtoto Nathan akawa anamfuatilia Eto’o kwa kila hatua akihama kutoka Hispania kwenda Italia, Urusi na sasa yupo England.
Ndoto kubwa ya Nathan ni kwamba siku moja aonane na Eto’o ana kwa ana, kitu ambacho wiki iliyopita kilitimia. Nathan alipata nafasi ya kwenda uwanjani Stamford Bridge Jumapili iliyopita kutazama mchezo wa Ligi Kuu England kati ya Chelsea na Manchester United. Kwenye mchezo huo, wenyeji Chelsea waliitandika Manchester United mabao 3-1.
Kitu cha bahati kwa Nathan ni kwamba shujaa wake, ambaye ni Eto’o alifunga ‘hat-trick’ kuing’arisha Chelsea uwanjani hapo. Baada ya kumshuhudia aking’ara uwanjani, siku chache baadaye mtoto Nathan alitembelea kwenye mazoezi ya Chelsea huko Surrey na akamwona shujaa wake, ambaye baadaye walifanya mazoezi ya pamoja.
Nathan, alifika kwenye viwanja hivyo vya Chelsea akiwa amevaa jezi ya Inter Milan iliyokuwa na jina la ‘Eto’o 9’ mgongoni. Akafanya mazoezi na staa huyo wa Cameroon kabla ya kupewa jezi nyingine ya Eto’o ya Chelsea yenye namba 29 anayovaa kwa sasa.
Mtoto Nathan alifika mazoezini hapo akiwa na wazazi wake, Mel na Debbie na mdogo wake wa miaka saba, Aiden.
Familia hiyo ilitazama mazoezi ya Chelsea kwanza kabla ya Eto’o kufanya mazoezi ya kivyake na mtoto huyo kwa kipindi cha dakika 20 katika uwanja wa ndani.
“Sifahamu ni nani aliyefurahi zaidi mimi au Nathan,” alisema Eto’o, baada ya kusaini mpira, jezi na kisha kumpa mtoto huyo kama zawadi.
Lakini, Eto’o pia aliipa mwaliko familia hiyo kwenda Stamford Bridge jana Jumapili kushuhudia mechi ya raundi ya nne ya Kombe la FA ambapo Chelsea ilitarajia kumenyana na Stoke City.
Baada ya kuifunga mabao matatu Manchester United, Eto’o alifichua jinsi alivyomshawishi kocha Jose Mourinho na kumwaanzisha kwenye mchezo huo licha ya kikosi hicho kuwa na mastraika wengine wakali, Fernando Torres na Demba Ba.
Eto’o na Mourinho walishawahi kufanya kazi pamoja wakati walipokuwa na kikosi cha Inter Milan ya Italia ambapo waliweza kunyakua mataji matatu kwa msimu mmoja, Serie A, Kombe la Italia na Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2010.
Kwenye kikosi cha Inter, Eto’o alikuwa akishirikiana na Diego Milito kwenye safu ya ushambuliaji iliyoifanya timu hiyo kuwa tishio na kuzitambia timu nyingi ikiwamo Barcelona iliyokuwa kwenye ubora wake kipindi kile.

No comments:

Post a Comment