Monday 20 January 2014

MAREKANI YAMUONYA TENA RAIS KAGAME WA RWANDA ....


WAKATI utata ukiwa umegubika juu ya kifo cha aliyekuwa Mkuu wa Usalama wa Rwanda, Kanali Patrick Karegeya, taarifa kutoka Ikulu ya Marekani zinaitaja nchi hiyo kuhusika moja kwa moja na kifo hicho. Msemaji wa Ikulu ya Marekani, Jen Psaki, amenukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari, ukiwamo mtandao wa Yahoo pamoja na BSN, akisema kuwa Rwanda imehusika na kifo cha Karegeya.

Katika maelezo yake hayo, Psaki alisema kwamba kwa mujibu wa onyo alilolitoa Rais Paul Kagame hivi karibuni, kwenye ibada ya kuliombea taifa hilo, inadhihirisha undani wa kifo cha Karegeya.

“Tuna wasiwasi na mfululizo wa mauaji ya wanasiasa maarufu nchini Rwanda,” alisema Psaki.

Kauli hiyo imekuja wakati tayari kumekuwapo na shutuma nyingi zinazomhusisha Rais Kagame na tukio la kifo cha Karegeya, kutokana na uhasama wa muda mrefu uliokuwepo baina yao.

Katika miaka ya hivi karibuni, uhusiano wa Rwanda na Marekani umekuwa ni wa mashaka, baada ya Rais Paul Kagame kuhusishwa na matukio mbalimbali ya kihalifu, yakiwamo mauaji ya wanasiasa wa upinzani pamoja na uchochezi wa vita katika eneo la Mashariki mwa Kongo.

Licha ya kukana kufadhili waasi wa M23, mwaka jana Rais Barack Obama alimuonya Kagame kuacha mara moja kuchochea mapigano Mashariki mwa Kongo.

Katika hotuba yake aliyoitoa hivi karibuni katika ibada ya kuliombea taifa hilo, Rais Kagame alitoa onyo kali kwa watu wanaoisaliti nchi hiyo kwamba watakabiliwa na wakati mgumu popote watakapokuwa.

Rais Kagame aliwataka Wanyarwanda wote kuungana katika kusimamia misingi sahihi na msimamo wao kama taifa, bila kujali tetesi zinazotoka katika mataifa ya nje kuhusu wale waliotangaza kuisaliti Serikali yake.

Hata hivyo, hakutaja moja kwa moja kuhusu tuhuma zinazoikabili Serikali yake juu ya mauaji ya aliyewahi kuwa Mkuu wake wa Ujasusi, Karegeya, ambaye ameuawa Januari Mosi, mwaka huu.

Kutokana na hali hiyo, kiongozi huyo wa Rwanda, alitoa onyo kali kwa kusema kuwa wale wote wanaoigeuka nchi yao na kuchagua kuua raia wasio na hatia kwa sababu zao binafsi, wanastahili kushughulikiwa ipasavyo.

Akisisitiza maelezo hayo, Kagame alisema hatakuwa na huruma na watu ambao wanasahau namna Rwanda ilivyowatengeneza hadi kufika mahali walipo.

Rais Kagame, aliwataka viongozi wa Rwanda kutosumbuliwa kwa yanayowakuta ‘maadui wa taifa’, kwa kuwa Mungu aliwapa nguvu ya kujenga na kukilinda kile walichokijenga, hivyo wale wanaosahau kwamba wana dhamana kwa Wanyarwanda na kuamua kutenda mambo mabaya dhidi ya taifa lao, ni wazi kwamba wamesahau kuwa hawataweza kuwa juu ya watu wao.

“Mliponiapisha kuwa kiongozi wenu mliniagiza kwamba wakati wote niilinde nchi hii, kwa maana ya kusimama kwa ajili ya watu wake,” alisema.

Hotuba hiyo iliibua mjadala mkubwa miongoni mwa watu ambapo wengi wao waliitafsiri kama ni ujumbe wa kilicho nyuma ya utata wa kifo cha Karegeya.

Kanali Patrick Karegeya (53), ambaye alikuwa akiishi uhamishoni nchini Afrika Kusini kwa miaka kadhaa, baada ya kutofautiana na mkuu wake wa zamani, Rais Kagame, aliuawa na watu wasiojulikana ambapo mwili wake ulikutwa katika Hoteli ya Michelangelo Towers, nchini Afrika Kusini.

Ikumbukwe kuwa Kanali Karegeya aliongoza Idara ya Usalama ya Rwanda kwa muda mrefu na alikuwa ni mtu aliyeaminiwa kwa kiasi kikubwa na Rais Kagame.

Hata hivyo, kiongozi huyo alijikuta akiingia katika uadui mkubwa hata kudaiwa kuwa Ofisa Usalama huyo alikuwa akiandaa mikakati ya kumpindua Rais Kagame.

Uadui huo haukuishia kwa Karegeya pekee, bali hata aliyekuwa Mkuu wa zamani wa Jeshi la nchi hiyo, Faustin Kayumba Nyamwasa na washirika wake, walikumbwa na hali hiyo, hivyo kuwalazimu kuikimbia nchi yao.

Serikali ya Rwanda imekuwa ikilaumiwa kwa kuwaua baadhi ya wanasiasa mashuhuri nchini humo, kama John Sengati, aliyeuawa nchini Rwanda, Kanali Theoneste Lizinde na Waziri wa zamani wa Rwanda, Seth Sendashonga waliouawa nchini Kenya.

Wengine ni Kanali Shabani Rutayisire, Gratien Munyarubuga, Dk. Assiel Kabera na Andre Kagwa Rwisereka ambao waliuawa nchini Rwanda.

Pia Regina Uwamaliya na Juvenal Uwilingiyimana nao waliuawa nchini Ubeligiji, huku Charles Ingabire akiuawa mjini Kampala na Pasteur Musabe aliyeuawa Cameroon.

Mpaka sasa kumekuwa na taarifa tofauti kuhusu kukamatwa kwa watu wanaoshukiwa kuhusika na kifo hicho, huku baadhi ya vyanzo vikimtaja mmoja wa wafanyabiashara wakubwa wa Rwanda, Apollo Gafaranga, ambaye alidaiwa kujenga urafiki wa karibu na marehemu Karegeya.

Oktoba mwaka jana, aliyekuwa mlinzi mkuu wa Rais Paul Kagame, Luteni Joel Mutabazi, alitekwa na kikosi cha Jeshi la Uganda na kukabidhiwa kwa Serikali ya Rwanda.

Luteni Mutabazi alikimbilia nchini Uganda Oktoba 2011, baada ya kufanikiwa kutoroka jela yenye ulinzi mkali wa kijeshi, iliyo katika mji wa Kami, nje kidogo ya mji wa Kigali, akituhumiwa kwa kuhusishwa na kutoroka kwa mkuu huyo wa majeshi na kukimbilia Afrika Kusini.

Mlinzi huyo pia anashutumiwa na Serikali ya Rwanda kwa kutoa siri kwa Kikosi Maalumu cha Umoja wa Mataifa chini ya Majeshi ya Umoja wa Kulinda Amani nchini Kongo, (MONUSCO) na kuwezesha kuchakazwa na kushindwa kwa kikosi cha waasi wa M23

No comments:

Post a Comment