Thursday 23 January 2014

NJIA INAYOWEZA KUPUNGUZA MAUMIVU WAKATI WA KUJIFUNGUA

NIMEWAHI kusoma habari za mkunga Kim Hildebrand Cardoso kutoka Berkeley, California nchini Marekani kuhusiana na uchungu waupatao wanawake wakati wa kujifungua na vifo vitokanavyo na uzazi. Ingawa sina cheti cha utabibu niliamua kujikita katika uchunguzi ili nijue kwanini akina mama wengi hasa Tanzania hupata matatizo wakati wa kujifungua?
Nilichogundua ni kwamba karibu kila msichana mwenye umri wa kuweza kubeba ujauzito anatambua matatizo ya mimba na maumivu makali wakati wa kujifungua, lakini miongoni mwa wanawake wenye kufahamu huo ni wachache wanaopewa elimu ya kupunguza uchungu wakati wa kujifungua na jinsi ya kudhibiti matatizo ya ujauzito.
Mpango wa hivi karibuni wa watalaamu wa nchini Marekani uliochapishwa na gazeti la The Daily Mail na The Daily Telegraph ulishauri kuongeza nasaha kwa akina mama wajawazito kwa lengo la kuwasaidia kupunguza hofu za uzazi zinazotajwa kuchangia kwa kiasi kikubwa kutokea kwa shinikizo la damu (blood pressure)  wakati wa kujifungua na hivyo kuongeza hatari ya mwanamke au mtoto kupoteza maisha.
Kliniki nyingi hapa nchini kwa mujibu wa uchunguzi wangu zimekuwa hodari kuwapatia wajawazito majibu yatokanayo na vipimo na kutojali umuhimu wa nasaha, jambo ambalo huwafanya wakina mama wengi kukosa elimu ya kutosha kuwasaidia. Lakini upande wa pili, wajawazito nao wamekuwa wakishindwa kuwasiliana barabara na wakunga kwa lengo la kujifunza juu ya uzazi salama.
Kitalaamu kujua jambo kunaongeza hofu hasa ujuzi huo ukikosa maelekezo ya ziada kuhusu kinga. Kwa mfano ni hatari zaidi kwa mwanamke kusikia tu kwamba wakati wa kujifungua huwa na maumivu makali bila kuambiwa anawezaje kuyapunguza. Katika hali ya kawaida mwili ulioandaliwa kupokea pigo fulani kwa mfano, hujenga hali ya kinga ambayo husaidia kupunguza maumivu.
Hii ina maana kwamba uchungu wa mwanamke aliyeandaliwa kisaikolojia kukabiliana na maumivu wakati wa kujifungua utatofautiana sana na yule ambaye mwili wake hakuandaliwa kushindana na uchungu huo. (Hakikisha hili kwa kujiandaa kupigwa na pigwa ghafla, kisha upime mshtuko na maumivu yake.)
Wanawake wengi wanaokumbwa na matatizo wakati wa ujauzito na kujifungua kwa mujibu wa uchunguzi uliohusisha majibu ya wakunga katika Hospitali za serikali za jijini Dar es Salaam, Tabora, Kigoma na Mwanza ni wale wa  uzazi wa kwanza. Sababu nilizozibaini mimi ni uhaba wa nasaha kama nilivyodokeza.
(Hapa nawaondoa wanaobeba mimba katika umri mdogo.)
Inaelezwa na wataalamu kwamba idadi kubwa ya wanawake wa kundi hilo wamekuwa wakipata aidha kifafa za uzazi au kushindwa kujifungua na hivyo kulazimika kufanyiwa upasuaji ili kuwanusuru na kifo. Matatizo yote haya yanatajwa kutokea nyuma ya shinikizo la damu ambalo nimeeleza habari zake hapo juu kwamba huchangiwa kwa kiasi kikubwa na hofu.
Ukiachana na kundi hilo la uzazi wa kwanza, uchunguzi unaonyesha pia akina mama wanaotoka kwenye familia zenye migogoro ya ndoa, waliotelekezwa baada ya kupewa ujauzito na wasiopendwa na jamaa zao wanaongoza kupata matatizo wakati wa kujifungua.
Hii inatoa sura kwamba ujauzito unahitaji zaidi faraja kuliko kitu kingine chochote.

No comments:

Post a Comment