Tuesday 28 January 2014

Ngeleja, Mpina, Mtanda waula Kamati za Bunge

 
Aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala Uchaguzi. Uteuzi huo ulitangazwa jana baada ya kamati mbalimbali za Bunge kufanya uchaguzi kujaza nafasi tisa zilizoachwa wazi na wenyeviti na wajumbe wa kamati hizo ambao wameteuliwa na Rais Jakaya Kikwete katika Baraza la Mawaziri.

Mbali ya Ngeleja ambaye anachukua nafasi ya Pindi Chana aliyeteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto.
Kabla ya hapo, Ngeleja ambaye ni Mbunge wa Sengerema (CCM) alikuwa Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, nafasi ambayo sasa imechukuliwa na Mbunge wa Karagwe (CCM), Gosbert Blandes.
Pia Mbunge wa Mchinga (CCM), Said Mtanda amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Jamii kujaza nafasi ya Jenister Mhagama aliyeteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Mtanda pia alikuwa Makamu mwenyekiti wa kamati hiyo kabla ya uchaguzi wa jana na nafasi yake imechukuliwa na Mbunge wa Mbinga Magharibi (CCM), John Komba.Mbunge wa Meatu (CCM), Luhaga Mpina amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi, Viwanda na Biashara nafasi ambayo ilikuwa ikishikiliwa na Mahmoud Mgimwa aliyeteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii. Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo anaendelea kuwa Mbunge wa Mkinga (CCM), Dunstan Kitandula.
Wazungumza
Akizungumzia uteuzi huo, Ngeleja alisema changamoto kubwa anavyokabiliwa nayo baada ya kuchaguliwa ni mchakato wa Katiba Mpya.
Alisema kamati yake ni mdau mkubwa wa mchakato huo na kwamba akishirikiana na wajumbe wake, wamepania kuona ikipatikana Katiba inayowakilisha masilahi ya watu wote.
“Hatutapenda kuona wanasiasa wanakuwa juu ya mchakato wa Katiba, tutahakikisha mawazo ya makundi yote yanaheshimiwa wakati wa mchakato huu,” alisema. Akizungumza baada ya kuteuliwa, Mtanda alisema: “Kazi kubwa iliyopo mbele yetu ni kupigania pensheni ya wazee, kukabiliana na changamoto za ajira kwa vijana pamoja na kuhakikisha kuwa Muswada wa Sheria ya Vyombo vya Habari unafikishwa bungeni na kujadiliwa.” Uchaguzi wa kamati nyingine ambazo wenyeviti na makamu wake wameteuliwa kuwa mawaziri utaendelea leo.
Pia Spika wa Bunge anatarajiwa kuwarejesha katika kamati mbalimbali mawaziri tisa ambao wameachwa na Rais Kikwete katika Baraza lake la Mawaziri.
Mawaziri hao ni wale watano walioachwa baada ya Rais Kikwete kufanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri na wengine wanne ambao alitengua uteuzi wao Desemba 20 mwaka jana baada ya wizara zao kutajwa kushindwa kusimamia Operesheni Tokomeza Ujangili.
Kwa mujibu wa kanuni za Bunge, Mbunge akiteuliwa kuwa waziri moja kwa moja anakuwa amepoteza sifa ya kuwa mjumbe wa kamati yoyote ya Bunge.

No comments:

Post a Comment