Saturday 18 January 2014

Pinda kuitia hasara Serikali

Uamuzi wa Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuruhusu malori makubwa ya mizigo yaendelee kuzidisha uzito wa mizigo, umetajwa kuwa ni hatari na utaisababishia Serikali hasara ya mamilioni ya fedha.
Hasara hiyo inatokana na uharibifu wa barabara za lami ambao unachangiwa kwa kiasi kikubwa na malori yanayozidisha uzito wa mizigo kinyume cha sheria na kanuni namba 7 (3) ya Sheria ya Usalama Barabarani ya 2001.
Ujenzi wa barabara ni wa gharama kubwa na hata ukarabati wake umekuwa ukitengewa mabilioni ya fedha za walipakodi kutokana na uharibifu unaofanywa.
Mathalani katika bajeti yake ya 2013/14, Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi, imetenga kiasi cha Sh314.535 bilioni kwa ajili ya mpango wa matengenezo ya barabara kuu na barabara za mikoa.
Kiasi hicho cha fedha ambacho ni zaidi ya robo ya bajeti nzima ya wizara hiyo kwa mwaka, kinatosheleza kujenga barabara mpya ya lami yenye urefu wa kilometa zipatazo 315, kwa makadirio ya kilometa moja kugharimu Sh1 bilioni. Katika mwaka huu wa fedha, bajeti nzima ya Wizara ya Ujenzi ni Sh1.226 trilioni.
Kauli ya Dk Magufuli
Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli, aliwahi kunukuliwa akisema ataendelea kusimamia sheria ya barabara namba 30 ya mwaka 1973, hadi anaingia kaburini kwa kuhakikisha hakuna magari ambayo yanazidisha uzito na kuharibu barabara.
“Nchini Ujerumani, uzito wa magari yote ni tani 40, Uingereza tani 40, Ufaransa 40, Urusi 38 lakini Tanzania tani 56, wakati mwingine tunakamata hadi tani 96,” alisema Dk Magufuli.
Hata hivyo, ujasiri wa Dk Magufuli ulizimwa na amri ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda, aliyetengua agizo la waziri huyo na kuamua kuruhusu magari yenye uzito uliopitiliza kuendelea kutumia barabara.

Mwananchi

No comments:

Post a Comment