Wednesday 29 January 2014

Simba yamruhusu Kapombe kusajili Yanga

BEKI Shomari Kapombe, yupo mjini Morogoro akifikiria jinsi ya kurudi katika klabu yake ya AS Cannes ya Ufaransa, lakini uchunguzi umeonyesha kwamba Simba, imebariki nyota huyo kutua Yanga au Azam FC endapo zitafikia makubaliano na Cannes.
Uchunguzi uliofanywa na Mwanaspoti, umebaini kwamba, kwa mujibu wa mkataba ambao Simba ilisaini na Cannes, wakati akiuzwa kupelekwa kwa Wafaransa hao ni kwamba beki huyo aliuzwa kwa klabu hiyo kwa mkataba wa miaka miwili.
Katika mkataba huo, ambao Mwanaspoti imepata sehemu ya nakala yake, uliosainiwa na Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage na Rais wa Cannes, Simba imemruhusu Kapombe kuuzwa kwa klabu  yoyote duniani endapo itafikia dau litakalohitajika, hatua ambayo inatoa fursa kwa klabu za Yanga, Azam FC Ashanti United na hata Galatasaray ya Uturuki kama zikimuhitaji.
Sehemu hiyo ya mkataba huo, inaonyesha kwamba endapo Kapombe atauzwa katika klabu yoyote duniani, Simba itavuna asilimia 40 ya mauzo hayo sambamba na Cannes ambao nao watapata mgawo kama huo, huku wakala wake Denis Kadito anayeishi Uholanzi akipata asilimia 20.
Wakala wa beki huyo, Kadito amezitaka klabu zinazomtaka mchezaji huyo kufuata utaratibu kwa kuzungumza na Cannes au yeye lakini kinyume na hapo zinajisumbua.

Mwanasipoti

No comments:

Post a Comment