Monday 27 January 2014

Wajilipue tu: Sababu za Man Utd kumuuza Rooney


MREMBO Coleen Rooney anasubiri kwa hamu kubwa mazungumzo ya mkataba mpya wa mumewe, Wayne Rooney wa kuendelea kubaki klabu Manchester United. Taarifa zinabainisha kwamba mchezaji huyo anaandaliwa mshahara wa pauni 300,000 kwa wiki.
Mrembo huyo anadaiwa kumtaka mumewe asaini mkataba mwingine wa miaka mitano wa kubaki Manchester ili kuwasubiri watoto wao; Kai, 4, na Klay mwenye umri wa miezi minane kuwa na umri mkubwa kabla ya kuhama.
Mkataba ambao Manchester United inataka kumpa Rooney una thamani ya pauni 65 milioni na utamfanya straika huyo kuwa mchezaji anayelipwa pesa nyingi zaidi England.
Kwa sasa analipwa kiwango sawa na mchezaji mwenzake wa Manchester United, straika wa Kidachi, Robin van Persie, pauni 250,000 kwa wiki.
Rafiki wa mrembo Coleen, 27, anasema: “Kitu kikubwa Coleen hataki wahame kutoka Kaskazini Magharibi na jambo hilo ni muhimu sana kwa Wayne. Hataki kuondoka eneo hilo na kutokana na kupokea ofa nzuri ya pesa nyingi anaamini hilo ni jambo muhimu akabaki klabu hapo.”
Manchester United imeipiga marufuku Chelsea kwamba isithubutu kumfuatilia straika wao huyo kwa sababu hawawezi kumuuza kwa wapinzani. Real Madrid pia inafukuzia saini ya staa huyo wa Old Trafford.
Lakini, Coleen hayupo tayari kuona watoto wake wakihamia London wangali wadogo hivyo, ukiweka kando Hispania. Anachotaka yeye waendelee kubaki Manchester hadi hapo baadaye.
Familia hiyo inaishi Prestbury, Cheshire, na wazazi wa Coleen, Colette na Tony wanaishi umbali wa maili 50 huko Formby, Merseyside, karibu na familia ya akina Rooney.
Coleen amesema Rooney, ambaye alijiunga na Manchester United akitokea Everton mwaka 2004, atapata shida sana kutulia kama atacheza bila ya sapoti ya familia zao.
Lakini, kuna mtazamo tofauti wakati kocha David Moyes akihaha na kuafiki mshahara wa pauni 300,000 kwa Rooney, wachambuzi wa soka wanadhani Manchester United inapaswa kulichukulia kwa hadhari suala la mchezaji huyo.

No comments:

Post a Comment