Monday 20 January 2014

Yanga yanasa Waarabu Uturuki

YANGA imetulia mjini Antalya, Uturuki ikipasha, na leo Jumatatu mchana itacheza dhidi ya Simurq PIK inayoshiriki Ligi Kuu nchini Azerbajain ikiwa ni mechi yake ya mwisho ya kirafiki nchini humo kabla ya kurejea Tanzania Alhamisi wiki hii.
Mabosi wazito wa Yanga waliopewa jukumu la kuiongoza klabu hiyo kwenye michuano ya kimataifa wamesisitiza kuwa asilimia kubwa ya kazi hiyo imekamilika na wameshanasa mikanda mitano yenye mbinu za Waarabu  ambapo wanacheza mechi mbili kwa wakati mmoja. Moja ya Wacomoro na ile ya Wamisri.
Yanga ambao wataingia kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika mwanzoni mwa mwezi ujao, wakianza na Komorozine ya Comoro jijini Dar es Salaam na watarudiana wiki mbili baadaye mjini Moroni. Endapo Yanga wakiwatoa Wacomoro hao, jambo ambalo si gumu watakwaana na Al Ahly ya Misri kwenye mechi ya raundi ya kwanza.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Kimataifa ya Yanga, Seif Ahmed ‘Seif Magari’ alisema kazi imeshaanza na walituma mashushu wao kimya kimya nchini Comoro na Misri.
Seif alisema mara baada ya kukabidhiwa majukumu hayo na baadaye kutoka kwa ratiba hiyo ya mechi za Ligi ya Mabingwa, kazi kubwa ilianza kwa siri na alilazimika kutuma mashushushu wake nchini Misri ambao walifanikiwa kupata mikanda ya mechi  za Al Ahly ambazo zote ni mechi za hivi karibuni na kwamba timu ikirudi kutoka Uturuki atamkabidhi kocha  Mholanzi Van der Pluijm mikanda hiyo.
Alisema mbali na ilichofanya kamati yake, Van der Pluijm naye amewaambia anajua mambo mengi kuhusu Al Ahly ikiwemo mifumo, staili zao za ushindi. Lakini wakati wakifanya hivyo wamehamishia majeshi yao kwa Wacomoro na hawataidharau mechi hiyo.
“Nina watu wakunisaidia kutekeleza majukumu haya, tumepata mikanda mitano ya mechi za Al Ahly, ipo mezani kwangu kwa sasa na itatusaidia, tutamkabidhi kocha na hata yeye kocha  ameshafanya kazi moja ya kupata mifumo yote ambayo inatumiwa na Al Ahly, ametutahadharisha na fitna za hawa Waarabu kwa sababu aliwahi kucheza nao mwaka jana,”alisema Seif.
“Moja ya jambo baya walilowahi kufanyiwa akiwa na timu yake ya Berekum Chelsea ya Ghana ni kupewa kadi nyekundu kwa mchezaji wao mmoja mapema sana, ametuonya tuwe makini sana. Watu wanaweza kuona kama tumewadharau hawa Wacomoro lakini hapana nao tupo katika hatua za mwisho kupata mikanda yao, kuna watu tumeshawapa hiyo kazi wapo kazini sasa.
“Wakikamilisha watawasilisha hiyo mikanda haraka,”alisema Seif kwa kujiamini huku akisisitiza kuwa vijana wake kwa sasa wapo nchini Comoro kwenye hatua za mwisho kabisa za kukamilisha majukumu yao.
Wakati Yanga wakifanya kazi hiyo,  Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limetoa majina ya waamuzi watakaochezesha mechi hiyo ya kwanza ya Yanga dhidi ya Komorozine waamuzi hao ni kutoka Somalia. Mwamuzi wa kati ni Hassan Mohamed Hagi wakati wasaidizi wake ni Hamza Hagi Abdi, Bashir Abdi Suleiman na Bashir Olab.  Kamishna wa mechi hiyo atakuwa Eugene Musoke kutoka Uganda.

Mwanaspoti

No comments:

Post a Comment