Tuesday 4 February 2014

Chadema wahoji uhusiano Tanzania, Rwanda


Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeiomba Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa inayoongozwa na Mbunge wa Monduli (CCM), Edward Lowassa kuunda kamati ndogo kuchunguza uhusiano kati ya Tanzania na Rwanda.
Chama hicho kimetoa ushauri huo baada ya baadhi ya vyombo vya habari nchini Rwanda kuripoti kuwa, viongozi wa Chama cha Upinzani cha Rwanda National Congress (RNC) na waasi dhidi ya Serikali ya nchi hiyo (FDLR) walifanya mazungumzo na Rais Jakaya Kikwete jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, taarifa hizo zilizoandikwa na gazeti la News of Rwanda ambalo linatajwa kuwa mshirika mkubwa wa Serikali ya nchi hiyo, takriban wiki mbili zilizopita, zilikanushwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Rwanda ambao ulifafanua kuwa tarehe iliyotajwa Rais Kikwete hakuwapo nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa chama hicho, Ezekiel Wenje alisema kamati hiyo inatakiwa kuchunguza taarifa hizo kwa sababu zinaweza kukwamisha juhudi za kuimarisha ushirikiano wa nchi hizo mbili.
“Mbali na kuomba Kamati ya Lowassa kuchunguza, pia tunaziomba mamlaka husika kuchunguza mchakato mzima wa utoaji wa hati za kusafiria ili kuhakikisha jina la Tanzania halitumiki vibaya,” alisema Wenje.
Alisema kuwa kuna haja ya Serikali kueleza msimamo wake kwa sababu Chama cha RDI tayari kimeshaeleza nia yake ya kuung’oa madarakani utawala wa Rais Paul Kagame wa Rwanda.

No comments:

Post a Comment