Monday 3 February 2014

Straika wa zamani Yanga auawa...


Pumzika kwa amani; Omar Changa wa tatu kutoka kushoto waliosimama akiwa na kikosi cha JKT Ruvu.
Hans Mloli na Lucy Mgina
MSHAMBULIAJI wa zamani wa Yanga na JKT Ruvu, Omari Changa, amefariki dunia jana.
Taarifa hizo mbaya kwa familia ya soka nchini, zilianza kusambaa jana jioni jijini Dar ambapo Championi Jumatatu lilifanya juhudi ya kumtafuta baba mzazi wa Omari, Changa Idd na kuthibitisha kwamba ni kweli mwanaye huyo ameaga dunia.
Imeelezwa kuwa mshambuliaji huyo ambaye mara ya mwisho alikuwa anakipiga Moro United inayoshiriki Ligi Daraja la Pili, aliokotwa maeneo ya Jangwani, Kariakoo akiwa ameshaaga dunia.
Mpaka sasa haijajulikana nini kilichosababisha kifo cha mchezaji huyo ambapo mzee Changa alisema kuwa amepewa taarifa mbili tofauti ambazo si rasmi kwamba amepigwa na watu huku wengine wakisema kuwa amepata ajali ya pikipiki.
“Mimi mwenyewe nilipata taarifa hizo kwenye saa 9 alasiri leo (jana) kwamba Omari amefariki ila sikuamini mpaka nilipoenda mochwari hospitalini Muhimbili kuhakikisha kama ni kweli.
“Nilipofika nilionyeshwa sura ya mwanangu pale mochwari ndipo nilipoamini kuwa ni kweli, nikaenda kuripoti polisi lakini nimeambiwa kesho niripoti saa 2 asubuhi baada ya hapo ndiyo tutajua taratibu za mazishi,” alisema mzee Changa aliyeonana na mwanaye mara ya mwisho siku tano nyuma zilizopita.
Aidha, mzee Changa alisema kuwa alimshuhudia mwanaye huyo akiwa na jeraha usoni lililopo kati ya jicho na pua.

No comments:

Post a Comment