Monday 3 February 2014

MCHEZAJI YANGA APIGWA PINGU...

Mshambuliaji wa Yanga, Shabani Kondo (kulia) akiwa ndani ya pingu.
Na Sweetbert Lukonge
MSHAMBULIAJI wa Yanga, Shabani Kondo, alionja joto ya jiwe jana baada ya kumkunja ofisa wa jeshi la polisi katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kisha kupelekwa kituo cha polisi.
Kondo alikumbana na mkasa huo kufuatia kutaka kupigana na askari baada ya mchezo dhidi ya Mbeya City ambao uliishuhudia Yanga ikivunja rekodi ya Mbeya kwa kuifunga bao 1-0.
Wakati mpira ulipomalizika, Kondo ambaye alikuwa jukwaani akiangalia mechi hiyo, alitaka kuingia katika vyumba vya kubadilisha nguo kwa nguvu, ndipo alipotokea askari na kumzuia lakini katika hali isiyotarajiwa, mshambuliaji huyo alianza ‘kutunishiana naye msuli’.
Baada ya kuona hivyo, askari huyo alimkamata Kondo, akampiga pingu kisha akamweka chini ya ulinzi, viongozi wa Yanga wakaingilia lakini polisi waliokuwa wamemzunguka wakakataa kumuachia.

Mshambuliaji wa Yanga, Shabani Kondo (wa kwanza kushoto) akiwa chini ya ulinzi.
Wachezaji wa Yanga walipoona mambo ni magumu kwa mwenzao, waliwazingira polisi ambao hata hivyo hawakulegeza kamba, badala yake wakampandisha kwenye Land Rover namba PT 2072 na kumkimbiza kituoni.
Hadi tunakwenda mitamboni, haikujulikana kama straika huyo alilala ndani au aliachiwa.
Hata hivyo mmoja wa askari polisi aliliambia gazeti hili kuwa mchezaji huyo wamemfungulia shitaka la kufanya fujo uwanjani pamoja na kuwatolea maneno ya kashfa askari wakati wakiwa kazini wakitekeleza majukumu yao.

GPL

No comments:

Post a Comment