Tuesday 4 February 2014

MC MAARUFU DAR APIGWA RISASI 9

Masikitiko yameigubika familia ya Jafari na wakazi wa Yombo-Kilakala, Temeke jijini Dar kufuatia tukio la mshereheshaji (MC) maarufu, Kelvin Jafari ‘Kalembo’ (42) kupigwa risasi tisa na watu wanaodaiwa kuwa ni majambazi.
MC Kelvin Jafari ‘Kalembo’ enzi za uhai wake.
Tukio hilo lilijiri saa moja usiku wa Jumamosi iliyopita huko Yombo ambapo kwa mujibu wa mashuhuda, MC huyo alipigwa risasi hizo akiwa anatokea ofisini kuelekea nyumbani kwake.
Waandishi wetu walifika kwenye msiba wa Kelvin na kuambiwa kuwa, marehemu aliponzwa na huruma kwani alimkuta kijana mmoja njiani akiwa ameporwa pikipiki na alimuomba awafuatilie kwa kutumia pikipiki aliyokuwa akiiendesha.
Ilidaiwa kuwa, marehemu alimbeba kijana huyo na kuwafuatilia waporaji hao ambapo walifanikiwa kuwakuta wakiiendesha pikipiki hiyo na kuwapita kwenda kusimama mbele yao kwa lengo la kuwazuia.
“Kumbe wale waporaji walikuwa na bunduki, wakamfyatulia MC risasi tisa mwilini,” kilisema chanzo chetu.
Ilidaiwa kuwa watu hao walimtambua kwa sura MC Kalembo na wakamtahadharisha kuacha kuwafuatilia lakini kabla marehemu hajawajibu akamiminiwa risasi.
Taarifa zinadai kijana aliyeporwa pikipiki alikimbia baada ya kumwona MC akianguka chini.
Habari zingine zinasema, marehemu kabla hajakata roho alichukua simu yake ya mkononi na kumpigia mtu aliyesemekana kuwa ni mshirika wake wa kikazi kwa lengo la kumjulisha kilichompata.
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Temeke, SACP Engelbert Kiondo alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa hadi sasa wanamshikilia mtu mmoja kuhusiana na tukio hilo.
Mwili wa marehemu ulipelekwa Kijiji cha Nangumbo. Ruangwa mkoani Lindi kwa mazishi Alhamisi iliyopita. Mungu ailaze pema peponi roho yake. Amina.

No comments:

Post a Comment