Tuesday 25 February 2014

Tunachojidanganya kuhusu Kaseja na Dida

SAYANSI ya soka la Tanzania ni tofauti na sayansi ya soka lolote ulilowahi kusikia duniani. Kuna wakati unajaribu kujiuliza tunatumia sayansi gani katika soka la kisasa lakini unaishia kukosa jibu.
Kwa mara ya kwanza nimesikia kuwa Tanzania kuna kipa wa mechi za ndani za ligi, na kuna kipa wa mechi za kimataifa. Hauwezi kuipata hii kokote duniani. Zamani na hata sasa tulizoea kusikia kipa wa dakika 90 na kipa wa kuja kucheza penalti baada ya dakika 120.
Lakini kuna sayansi mpya ya kipa wa mechi za kimataifa na kipa wa mechi za ndani. Ndivyo wanavyojidanganya watu wa benchi la ufundi au viongozi wa Yanga. Kwamba Juma Kaseja ni kipa waliyemsajili kwa ajili ya mechi za kimataifa wakati Deogratius Munishi ‘Dida’ ni kipa waliyemsajili kwa ajili ya mechi za ndani.
Katika soka halisi hakuna kitu kama hiki. Kipa wa mechi za ndani anapaswa kucheza mechi za kimataifa kwa sababu anacheza mechi nyingi kila mwisho wa wiki na ni rahisi kuwa fiti kuliko kipa wa mechi za kimataifa.
Kipa wa mechi za kimataifa anacheza mechi nne au sita tu kwa mwaka. Tangu lini kipa akacheza mechi chache kama hizi na akawa fiti kama si kumtafutia lawama?
Na hii si kwa kipa tu, bali kwa mchezaji yoyote uwanjani.
Kama Yanga wanataka kufanya vizuri katika mechi zao za kimataifa ni bora waendelee kumtumia Dida kwa sababu wakimtumia Kaseja watajikuta wanamlaumu bila ya sababu za msingi kwani naye anahitaji mazoezi yenye ushindani ili kulinda kipaji chake jambo ambalo kwa sasa analikosa .
Na kama wanataka Kaseja awe kipa wa mechi za kimataifa, basi huu ni wakati wa kuanza kumpanga mechi za ndani ili aendelee kuchangamka langoni.
Barani Ulaya, kipa wa kwanza anabakia kuwa kipa wa kwanza tu kwa sababu kadri anavyokumbana na mikikimikiki langoni ndivyo anavyoendelea kuimarika.
Kadri kipa yeyote anavyokaa nje ndivyo anavyoendelea kuporomoka kiwango chake taratibu bila ya kujifahamu.
Katika pambano la Jumamosi dhidi ya Al Ahly natazamia Kaseja kutocheza vema kama akipangwa kwa sababu uzoefu pekee hausaidii kiwango kizuri cha mchezaji.
 Mikikimikiki ya kila wiki inasaidia zaidi wachezaji hasa wa nafasi ya kipa. Kwa mshambuliaji haliwi tatizo kubwa sana.
Sir Alex Ferguson aliwahi kutaka kuwabadili makipa wake, David de Gea na Anders Lindergaard kadri awezavyo lakini mwisho wa siku alilazimika kukubali ukweli kwamba De Gea angecheza mechi karibu zote za Manchester United akiwa chaguo namba moja katika kikosi cha kwanza.
Na labda kwa ushauri mwingine kwa watu wa Yanga ni kwamba hawana sababu yoyote ya kumuharibia maisha kipa wao wa tatu, Ally Mustapha ‘Barthez’.
Huu ni wakati mwafaka wa kumruhusu kipa huyo aondoke klabuni kwao hata kama ana mkataba nao. kwani hawamtumii na hivyo anahitaji changamoto kupitia klabu nyingine ambazo zinahitaji huduma yake.
Kwa eneo la golikipa, daima unapaswa kuwa na makipa wawili wakubwa kama Dida na Kaseja. Kipa wa tatu anapaswa kuwa kipa kijana ambaye atakuwa ana maisha marefu klabuni huku akijifunza kutoka kwa wawili waliopo.
Kwa ilivyo sasa, Barthez hana cha kujifunza kutoka kwa Kaseja wala Dida. Hapo hapo unajaribu kuwaza kuwa kama Kaseja anasugua benchi vipi kwake yeye?  Uungwana mzuri sana ni kumruhusu aondoke kwenda kucheza katika timu ambayo atapangwa mara kwa mara.

Mwanaspoti

No comments:

Post a Comment