Monday 3 February 2014

Serikali yaja na mapya katika elimu

 
Serikali imeanzisha mfumo mpya wa udahili kwa wanafunzi wanaoingia kidato cha kwanza, kwa kuwalipia ada watakaojiunga na shule binafsi.

Vilevile, imeanzisha utaratibu utakaoshirikisha shule binafsi na zinazoendeshwa na Serikali katika kuteua wanafunzi watakaojiunga na sekondari.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome, alisema kuwa utaratibu huo unatarajiwa kuanza kutumika pia kwa wanafunzi wanaotarajiwa kuingia kidato cha tano mwaka huu.
Alisema kuwa mfumo huo utasaidia kuwezesha wahitimu wengi, waliofanya vizuri kupata nafasi za kuendelea na masomo huku pia shule nyingi zikiwa na uhakika wa kupokea wanafunzi.
“Tunajua kumekuwa na tatizo la shule nyingi kukosa wanafunzi zikiwamo za Serikali kwa kuwa wapo wanafunzi ambao huchaguliwa kujiunga na shule za Serikali, lakini wazazi wao huwapeleka kwenye shule binafsi,” alisema Profesa Mchome na kuongeza;
“Vilevile, kuna watoto ambao hushindwa kuendelea na masomo ya sekondari licha ya kufanya vyema kama ilivyotokea kwa mwaka huu kutokana na uchache wa madarasa.”
Profesa Mchome alitoa mfano wa kujitokeza kwa tatizo hilo mwaka jana akisema kuwa idadi kubwa ya wanafunzi waliomaliza darasa la saba na kupata matokeo mazuri, walikosa shule, hivyo kulazimika kusubiri uteuzi wa pili, wakati wenzao tayari wameshaanza masomo.
“Lakini chini ya utaratibu huo wa udahili wa pamoja, Serikali imekusudia kuweka utaratibu maalumu utakaowawezesha baadhi ya wanafunzi kuendelea na masomo kwenye sekondari binafsi kwa utaratibu maalumu wa malipo,” alisema Profesa Mchome.
Aliwatoa wasiwasi watu walio na tabia ya kubeza shule za Serikali zinazolalamikiwa kuwa na matokeo mabaya kwenye mitihani mbalimbali ya taifa, akisema kuwa hata shule binafsi zimekuwa zikishika nafasi ya mwisho.
“Hadi sasa elimu inayotolewa nchini kwa ubia na sekta binafsi bado haijafikia kwenye kiwango cha ubora, kwani hata kwa shule binafsi zipo zinazofanya vibaya, ikilinganishwa na za Serikali,” alisema.
Profesa Mchome aliongeza: “Zipo shule za sekondari za Serikali zinazofanya vizuri kama vile Kilakala na Ilboru.”
Alibainisha kuwa Serikali imekusudia kuziimarisha shule zake kongwe nchini ili ziwe na majengo bora, maabara zenye vifaa na walimu wa kutosha.

Alifafanua kwamba mpango wa kuboresha shule hizo unatarajiwa kuanza mwaka huu wa fedha na kwamba utarejesha heshima ya kitaifa na kurudisha dhana ya kuanzishwa kwa shule hizo.
”Vitakuwa ni vituo bora ingawa hii haipo kwenye mpango wa Matokeo Makubwa Sasa, lakini ni mpango wetu wa pili. Pia tunatarajia tutashuka katika ngazi ya mkoa kwa kujenga shule nzuri katika kila mkoa ambao hauna shule kongwe,” alisema Profesa Mchome.
Alieleza kuwa wanatarajia kushuka hadi ngazi ya wilaya baada ya kuziimarisha sekondari za mkoa na kwamba hatua hiyo ipo katika mpango endelevu wa Serikali.
Mchome alisema kwamba awali, Serikali ilikusudia kuanza kuutumia utaratibu huo kwa wanafunzi waliomaliza darasa la saba mwaka jana, lakini ilishindikana kutokana na wamiliki wa shule binafsi kutaka muda zaidi wa kuelimishwa.
Akizungumzia utaratibu huo Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi (Tamongsco), Mahmoud Mringo alisema kuwa Serikali imeshawasilisha dhamira hiyo, lakini haijaweka wazi utekelezaji wake.
Alisema kuwa utaratibu huo hautakuwa na matatizo endapo kutakuwapo usawa na wanafunzi kupewa fursa ya kuchagua shule kama ilivyo kwa vyuo vikuu .
“Mpango siyo mbaya ila tunachotaka ni ushirika wa sawa kwa sawa. Shule ziwekwe kwa pamoja na mwanafunzi apewe nafasi ya kuchagua kama inavyofanyika katika vyuo vikuu na siyo kuwachukua wanafunzi waliokosa nafasi serikalini,” alisema Mringo.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Ezekiah Oluoch alisema kuwa mpango huo hauwezi kuwa na manufaa katika elimu kutokana na kutaka kuwanufaisha watendaji wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi aliodai wengi wao ndiyo wamiliki wa shule binafsi.
Alidai kwamba kutaka fedha katika shule zao ndiyo sababu ya watendaji na wanaofanya uamuzi katika sekta ya elimu kuleta mpango huo ambao alisema kuwa mwisho wa siku utaibua mgogoro mkubwa.
“Mfumo kama huu ulijaribiwa katika nchi za Amerika Kusini, lakini ulishindikana kwa sababu ni mfumo mbovu, unachangia kuibua migogoro kwenye jamii. Tatizo ni kwamba, watoa uamuzi katika sekta hii ndiyo wamiliki wa shule binafsi,” alisema Oluoch akidai na kuongeza;
“Upande wa CWT hatujashirikishwa katika hili na sisi tunalisikia, lakini mpaka sasa tunaona haufai kabisa kwa maendeleo ya elimu nchini.”

No comments:

Post a Comment