Tuesday 4 February 2014

Chelsea yaipasua Man City uwanjani kwao Etihad


JOSE Mourinho hatari sana. Utasema nini zaidi ya hicho baada ya jana Jumatatu usiku kumzidi mbinu Manuel Pellegrini kwa kumpangia kikosi kijanja na kuisambaratisha Manchester City kwao kwa bao 1-0 katika mchezo wa Ligi Kuu England na hivyo kutibua rekodi ya wenyeji wao uwanjani Etihad.
Bao la shuti kali la beki wa kulia, Mserbia Branislav Ivanovic kwenye dakika 32 lilitosha kumtoa kimasomaso Mourinho na kikosi chake cha Chelsea na hivyo kufanikiwa kuitambia Manchester City katika mechi zote mbili ilizocheza na timu hiyo kwenye Ligi Kuu.
Kwenye mchezo huo, Chelsea iliyocheza kwa nidhamu kubwa ilistahili kushinda baada ya kufanya mashambulizi ya nguvu kwenye goli la Manchester City na kugongesha mwamba mara tatu kupitia kwa Samuel Eto’o, Nemanja Matic na Gary Cahill.
Chelsea ilikuwa na nafasi kubwa ya kushinda mabao mengi kwenye mchezo huo kwa sababu walikuwa tishio muda wote, huku kiungo wao Mbelgiji, Eden Hazard akicheza kwa kiwango cha juu sana. Lakini, pongezi kubwa ni kwa Mourinho aliyeingia na kikosi cha kijanja sana.
Kwenye mchezo huo, Mourinho alianza na straika mmoja tu, Eto’o, lakini alichokuwa akikifanya staa huyo wa Cameroon ni kuwakaba mabeki wa kati wa Manchester City na kuwanyima uhuru wa kupandisha mipira mbele. Kwenye kiungo Manchester City ilimkosa kiungo wake muhimu,
Mbrazili Fernandinho huku Mourinho akiwaandisha wachezaji wawili wakabaji, David Luiz na Matic, ambao walikuwa na kazi moja tu ya kutibua mipango ya wapinzani wao pamoja na kumvuruga Yaya Toure.
Mreno Mourinho alitumia mbinu sana baada ya kumtumia Ramires kama mkabaji wa kuanzia mbele akishrikiana na Eto’o jambo lilimfanya Hazard kuwa huru na kupanga mashambulizi ya kikosi hicho cha Chelsea.
Matokeo hayo yalikuwa ya kwanza kwa Manchester City kwenye mechi 61 wakicheza nyumbani bila ya kupata bao tangu Novemba 2010.
Jinsi bao lilivyofungwa
Pasi fupi ilitoka kwa Eto’o, ambaye alipiga nyuma kwa Azpilicueta. Azpilicueta alituliza na kupiga pasi ndefu kwa Hazard, aliyekuwa upande wa kushoto.
Mbelgiji huyo alikokota mpira kuingia nao kwenye goli la Manchester City na kupiga pasi kwa Ramires, ambaye alimgongea Ivanovic na yeye akampenyezea Hazard tena. Hazard safari hii alikuwa upande wa kulia, alipiga krosi kwa Ramires kabla ya mpira kumfikia Ivanovic aliyefumua shuti kali la chinichini lililomshinda kipa Joe Hart na kutinga wavuni.
Kwa bao hilo limeifanya Chelsea kukusanya pointi tatu muhimu na sasa awamefikisha pointi 53 sawa na Manchester City wakiwa wamezidiwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Mwanasipoti

No comments:

Post a Comment