Friday 7 February 2014

Waziri amtisha Rais Yoweri Museveni

Waziri wa Serikali za Mitaa nchini Uganda, Alex Onzima ametishia kujiuzulu wadhifa wake iwapo Rais Yoweri Museveni hatakubali kutia saini muswada unaohusu wapenzi wa jinsia moja.
Muswada huo uliopitishwa na Bunge la nchi hiyo mwishoni mwa mwaka jana unatoa adhabu kali kwa wale watakaobainika kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja, suala ambalo limekuwa likipingwa na baadhi ya mataifa ya Ulaya ambayo yamekuwa yakitishia kusitisa utoaji wa misaada ya kumaendeleo iwapo utatiwa saini.
Akizungumza na wanahabari kwenye hafla ya kusimikwa kwa mkuu wa Diakonia ya Maracha katika kijiji cha Nyoro, Onzima alisema hana namna kwa kuwa hajapata nafasi ya kumweleza lolote Rais Museveni kuhusu muswada huo.
“Museveni anatakiwa aangalie kwa kina mambo muhimu kwenye muswada huo. Yeyote aliyeko hapa ambaye anaripoti kwake aende na amweleze kwamba sikubaliani hata kwa nukta moja katika suala hili hata kama itakuwa ni kwa gharama ya kupoteza nafasi yangu ya uwaziri, nina makazi yangu hapa Maracha,” alisema.
Hii ni mara ya kwanza kwa mtumishi wa juu wa Serikali kuzungumza hadharani kupinga hatua ya Rais Museveni kuchelewa kupitishwa muswada huo uliopitishwa Desemba 23 mwaka jana kuwa sheria. Waziri huyo alimsifu Rais wa Senegal, Macky Sall kwa hatua yake ya kumweleza Rais Barack Obama wa Marekani wakati wa ziara yake nchini humo mwaka jana kwamba suala la wapenzi wa jinzia moja halina nafasi kwa Afrika.
“Hebu fikiria iwapo Rais Obama angeotembelea Uganda na kumuuliza Museveni kuhusu suala la wapenzi wa jinsia moja, hivi nini kingetokea?” alihoji.
Waziri huyo amekuwa ni mmoja wa mawaziri ambao wamekuwa wakipinga hatua ya Serikali kuchelewa kutoa uamuzi katika masuala mengi, ambapo wakati fulani aliamua kujitoa kwenye chama tawala cha National Resistance Movement (NRM) na kujiunga na Reform Agenda mwaka 2001.
Baada ya kushiriki huko na kwua mpinzani wa Serikali kwa muda, alirejea na kujiunga na NRM mwaka 2011 ambapo baadaye aliteuliwa na rais museveni kuwa miongoni mwa mawaziri katika baraza lake.

No comments:

Post a Comment