Monday 3 February 2014

Fifa: Tunamchunguza Okwi

WAKATI Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), likisubiri majibu ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), juu ya hatima ya usajili wa mshambuliaji wa Yanga, Emmanuel Okwi, Fifa wamekiri kuwa na vielelezo vya Okwi na watatoa ufafanuzi.
Msemaji wa Fifa, Alois Hug, ameliambia Mwanaspoti jana Jumapili kwamba tayari wameshapokea barua ya TFF, wakiomba kupatiwa ufafanuzi juu ya usajili wa mshambuliaji huyo raia wa Uganda na muda mwafaka watatoa jibu.
Hug alisema baada ya kupokea barua ya TFF, wameanza kuifanyia kazi kwa kuipeleka katika kitengo kinachohusika na usajili ili kupatia majibu yatakayotoa hatima ya Okwi kuitumikia Yanga.
Alisema, kwa sasa hawezi kutoa jibu lolote kuhusu hatima ya mshambuliaji huyo ambaye Simba ilimuuza katika klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia mapema mwaka jana kabla ya mchezaji huyo kuondoka Tunisia akidai kutolipwa haki zake na kurudi klabu yake ya awali ya Sports Club Villa ya Uganda iliyomuibua.
Hata hivyo akiwa Villa, Okwi alisajiliwa na Yanga, usajili uliokuwa kiini cha utata kati ya mchezaji huyo na klabu ya Simba ambayo bado inaidai Etoile na kuifanya TFF itafute ufafanuzi kutoka Fifa.
“Tunachoweza kukuthibitishia ni kwamba Fifa tumeshapokea barua kutoka TFF wakiomba ufafanuzi juu ya usajili wa Okwi.” kwasasa hatuwezi kusema lolote mpaka ufafanuzi utakapotolewa,” alisema.

No comments:

Post a Comment