Thursday 6 February 2014

Kikwete awaonya wanasiasa

 
Rais Jakaya Kikwete ametangaza kuwa Bunge Maalumu la Katiba litaanza Februari 18 mwaka huu huku akiwataka viongozi wa vyama vya siasa nchini kuweka mbele masilahi ya Taifa na siyo ya vyama vyao.


Rais Kikwete alisema wajumbe 640 wa Bunge hilo wengi ni wafuasi wa vyama vya siasa, hivyo wanatakiwa kukubaliana kwa hoja badala ya kila upande kuvutia kwake.
Aliwaonya pia wanasiasa kutokazania suala la muundo wa Muungano peke yake, bali waangalie na masuala mengine yaliyomo kwenye rasimu hiyo ambayo ni muhimu kwa Taifa.
Bunge la Katiba linafanyika baada ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kukamilisha kazi yake ya miezi 20 kukusanya maoni ya wananchi na kuandaa Rasimu ya pili Katiba ambayo ilitolewa Desemba 30, mwaka jana.
Akizungumza na viongozi mbalimbali wa vyama hivyo jana katika mkutano wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini, Rais Kikwete alisema kama wanasiasa wakikubaliana, hakuna mwananchi yeyote atakayepinga uamuzi utakaopitishwa na Bunge hilo.
“Nimeshauriana na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein kuwa Bunge Maalumu la Katiba lianze vikao Februari 18, mwaka huu. Bunge hili litafanyika kwa siku 70 na kama mambo yatakuwa hayajamalizika zinaweza kuongezwa siku 20,” alisema Rais Kikwete.
Aliongeza: “Nyinyi ndiyo wenye jukumu la kuipatia nchi yetu katiba nzuri inayojali masilahi ya watu wake ndani ya pande zote za Muungano, kuanzia watu wanapoishi, wanapotoka na asili yao. Msije mkafanya uamuzi utakaowaingiza katika uadui na chuki.”
Katika hotuba yake ya dakika 70, Rais Kikwete alisema yapo mambo mengi ya kujadili katika Bunge hilo, siyo muundo wa Muungano pekee.
“Mnakwenda kuijadili Katiba kuhusu masuala mbalimbali yenye masilahi ya nchi yetu, siyo mambo ya Muungano tu. Wekeni utaratibu ili muweze kukubaliana hata katika masuala ambayo kila mmoja ana msimamo wake,” na kuongeza:
“Kuna suala la ukomo wa kugombea ubunge kuwa vipindi vitatu. Hii maana yake ni kuwa kama umeshakuwa mbunge kwa vipindi vitatu huwezi kugombea hata urais,” alisema na kuongeza;
Kwa mujibu wa Rasimu ya Kwanza ya Katiba, Ibara ya 75 (e) mgombea urais alitakiwa kuwa na sifa za kugombea ubunge, ikiwamo ya kutowahi kuwa mbunge kwa vipindi vitatu. Hata hivyo kwenye Rasimu ya Pili itakayojadiliwa na Bunge hilo, ibara ya 79 inayozungumzia sifa za kuwania urais, hailazimishi mgombea urais kuwa na sifa za kuwania ubunge.
Rais Kikwete alisema wanasiasa wana dhamana ya kuwapatia Watanzania Katiba itakayodumu kwa miaka 50 ijayo na kuimarisha Muungano, umoja, amani na utulivu, siasa safi na kuongeza kasi ya maendeleo na ustawi wa wananchi.

Mwanachi

No comments:

Post a Comment