Tuesday 25 February 2014

Viongozi wa Simba wamepata msiba wa mjomba yupi?

UMEWAHI kuona rubani anaiteka ndege yake? Bila shaka unakumbuka kisa cha rubani msaidizi, Hailemedhin Abera (31) aliyeiteka ndege ya Ethiopian Airlines Jumatatu ya wiki iliyopita kwa madai ya kuwa na msongo wa mawazo kwa kufiwa na mjomba wake.
Abera, ambaye amefanya kazi kwenye shirika hilo maarufu la ndege kwa miaka mitano alijifungia kwenye chumba cha marubani baada ya rubani mkuu kwenda msalani.
Rubani huyo msaidizi ‘aliendesha’ ndege hiyo kwa saa sita na badala ya kuipeleka Roma, Italia aliipeleka Geneva, Uswisi ambako alitua baada ya kuomba kupewa hifadhi nchini humo.
Rubani huyo alifanya kituko kwa kuwatisha abiria kwa kuchomoa vikasha vya hewa ya oksijeni kwenye ndege hiyo na kutishia kuzima mfumo wa hewa iwapo abiria hao wasingekubali kufuata maelekezo yake.
Rubani huyo akawaambia abiria kwa ukali: “Kaeni chini, vaeni vikasha vya oksijeni kwenye viti vyenu, nitakwenda kukata mfumo wa hewa ya Oksijeni.”
Baada ya rubani huyo kuwazungusha abiria kwa saa sita angani wakiwa hawajui hatima yao, alitua Geneva na kushuka kupitia dirishani kwa msaada wa kamba huku akiomba hifadhi kabla ya kujisalimisha kwa polisi.
Ndege hiyo aina ya Boeing 767-300 iliyokuwa na abiria 201 na wahudumu iliondoka mjini Addis Ababa na kutua mjini Geneva, ikiwa imebakiza mafuta yanayayoiwezesha kuendelea kuwepo hewani kwa dakika 20 tu.
Si ndege tu ambayo inaweza kutekwa, hata viongozi wa Simba wamewateka nyara wanachama wao kwa kuitisha mkutano mkuu Machi 16 ambao utajadili ajenda moja tu ya mabadiliko ya katiba.
Itakuwaje Simba yenye migogoro mingi iwe na ajenda moja tu ya kujadili mabadiliko ya katiba wakati wanachama wanataka kujua suala la uwanja wao wa Bunju B.
Itakuwaje ijadiliwe ajenda moja tu katika mkutano huo wakati wapo baadhi ya wanachama katika Simba ambao wanataka kujua Emmanuel Okwi aliuzwa vipi kwenda Etoile du Sahel ya Tunisia  bila malipo yoyote.
Wanachama wanataka kupata majibu inakuwaje Okwi licha ya ubora wake auzwe kwa mkopo na fedha haijalipwa mpaka sasa?
Wanachama wanataka kujua inakuwaje mchezaji wao kiraka Shomari Kapombe apelekwe AS Cannes ya Ufaransa kwa mkataba ambao hauna maelezo ya kujitosheleza.
 Kapombe, miongoni mwa wachezaji bora Afrika Mashariki na Kati sasa yupo nchini akiwa hajui hatima yake, lakini Simba wapo kama vile hawana shida naye.
Simba imecheza mechi nne na kupata pointi mbili tu, kuna tatizo gani hapo. Wanachama wanataka kupata majibu sahihi kuna tatizo gani katika timu hiyo?
Matatizo yote hayo yanapaswa kujadiliwa katika mkutano mkuu wa wanachama wa Simba na hasa ikizingatiwa kuwa kuna mgawanyiko mkubwa ndani ya uongozi na Kamati ya Utendaji.
Kwa misimu miwili mfululizo, Simba inashindwa kushiriki mashindano ya Shiriisho la Soka Afrika (CAF) iwe Ligi ya Mabingwa au Kombe la Shirikisho. Wanachama wanataka kujadili hayo.
Inawezekana Simba inataka kufika mahali fulani kuzuri, lakini viongozi wake wamewateka wanachama na wanawapeleka sehemu nyingine huku wakiomba hifadhi maalumu.
Yule rubani wa Ethiopia aliiteka ndege kwa madai alikuwa na msongo wa mawazo baada ya kufiwa na mjomba wake, sielewi viongozi wa Simba wamepata msongo wa mawazo baada ya kufiwa na mjomba yupi?

Mwanaspoti

No comments:

Post a Comment